Jamani hata ng'ombe anayesubiri kuchinjwa hutunzwa!
WIKI hii Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Robert Kisanga, alitoboa siri iliyojificha kwa muda mrefu nchini kuhusu maisha ya wafungwa na mahabusu katika magereza.
Alisema tume yake imebainisha kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika magereza nchini ambako wafungwa na mahabusu watoto wanawekwa pamoja na watu wazima hali inayosababisha kulawitiwa.
Hata hivyo, Jaji Kisanga alisema tume hiyo ilisema kuwa kumekuwa na usiri mkubwa katika suala zima la ulawiti baina ya wafungwa na maafisa wa Magereza.
Alisema kutotengwa sehemu kwa watoto wadogo na watu wazima, limeelezwa kuwa ndicho chanzo cha ulawiti magarezani na hivyo kuathiri juhudi za mapambano dhidi ya ukimwi magerezani na kwamba kumejitokeza usiri juu ya suala la kulawiti katika pande zote maafisa wa Magereza, wafungwa na mahabusu wenyewe.
Maelezo ya Jaji Kisanga ni matokeo ya ziara ya Tume ya kukagua Magereza na kambi za Magereza 15 na vituo vya polisi 42 katika wilaya 20 za Tanzania Bara kwa mwaka 2004/2005.
Miongoni mwa Magereza na kambi zilizokaguliwa ni pamoja na Kongwa, Mpwapwa mkoani Dodoma, Muleba (Kagera), Kilosa (Morogoro), Magu, Butimba (Mwanza), Kahama na Shinyanga.
Katika magereza 15 yaliyokaguliwa na Tume ni gereza la Kongwa (Dodoma) tu ambalo lina bweni la watoto, yaliyobaki watoto waliwekwa katika chumba kimoja na watu wazima, hali hiyo ni ukiukwaji wa haki za watoto na pia inahatarisha maisha ya watoto kisaikolojia.
Pia magereza hayo yaliyotembelewa na kukaguliwa zaidi ya asilimia 50 yalikuwa na msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu na kwamba hali hiyo inahatarisha maisha na ni uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Kwa hakika ripoti hiyo inatufumbua macho kujua hali ya magereza yetu yalivyogeuka kuwa jehanamu badala ya kuwa eneo la kurekebisha tabia za wafungwa.
Hivi sasa mtu akipatikana na kosa hata la kuiba chungwa akifungwa jela miezi sita ni sawa na amefungwa kifungo cha maisha kwa vile huwa hana uhakika kama anatarejea salama au atakufa kutokana na mazingira mabaya yaliyopo katika magereza.
Vitendo na mazingira yaliyoelezwa na tume ya Jaji Kisanga kwamba mahabusu watoto na wafungwa wakubwa kuwekwa katika chumba kimoja kwa hakika ni ni cha hatari na kinahatarisha maisha ya watoto hao.
Nashindwa kuelewa uamuzi huo wa kuwachanganya mahabusu watoto na wafungwa wakubwa unafanywa kutokana na na nini? Ni uhaba wa vyumba vya magereza kutunzia wafungwa au kitu gani? Nadhani waziri wa Mambo Ndani ya Nchi, John Chiligati anapaswa kutueleza watanzania.
Mbali ya kulawitiwa watoto katika magereza lakini hata hali ya magereza bado haziridhishi. Magereza mengi vyumba vya mahabusu vingi vina mwanga mdogo kutokana na kuwa na madirisha madogo au kutokuwa na madirisha kabisaa.
Pia vyumba hivyo mbali ya kutokuwa na mwanga lakini ni vidogo ambavyo wafungwa wanalala wengi wakiwa wamekaa kutokana na kukosa nafasi pamoja na kujisaidia katika ndoo jambo ambalo limekuwa likisababishia wafungwa hao kupata magonjwa wa milipuko kama kipindupindu na kuhara damu.
Hivi kweli hata kama wafungwa ni wahalifu ni haki kuwaweka katika chumba ambacho hakina mwanga na kidogo ambacho hawezi hata kulala. Kwa maana nyingine ni kwamba mtu akikaa mahabusu kwa miaka mitatu atakuwa hawezi kupata sehemu ya kulaza ubavu wake katika kipindi chote hicho? Hii ni njia bora ya kuwarekebisha tabia wafungwa kweli ili wakitoka wawe raia wema au ni njia ya kuwaua?
Kwa maana nyingine ni kwamba wafungwa na mahabusu wa Tanzania wanatumikia adhabu mara mbili ya kwanza ya kutokana na makosa waliyoyafanya na mazigira mabaya yaliyopo katika vyumba vya magereza.
Hata hadithi ya maarufu ya safari za Sindbad alipofika katika kisiwa cha wala watu walipokelewa kwa heshima na wenzake wakalishwa mapande ya nyama makubwa ili wanenepe kabla ya kuliwa.
Bahati yake Sindbad alikataa kuyala akakonda na kuonekana hafai kuwa chakula wa mfalme wa eneo hilo. Kwa maana nyingine hata kama waandhibiwa lakini utu wao kama binadamu unabaki pale pale.
Nadhani kufikiria kuwa kuweka mazingira ya magereza katika hali nzuri ni kuwafanya watu waendelee kufanya uhalifu ni makosa kwa vile kunyimwa uhuru aliokuwa nao wa kuwa uraiani, kuwa mbali na familia yake, ndugu zake, marafiki na kufanya kazi akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari magereza ni adhabu tosha inayomfanya mtu akitoka kule amerekebishwa tabia yake.
Badala ya magereza nchini kuwa chuo cha mafunzo ya kurekebisha tabia hivi sasa yamekuwa ni kituo cha kupika wahalifu na wengi kufa wakiwa wanatumikia vifungo vya kutokana na kuugua ugonjwa mbalimbali yakwamo ya kifua, kikuu, ukimwi na kipindupindu.
Nadhani sasa umefika wakati kwa serikali iboreshe hali ya magereza yetu ili kweli yawe ni vyuo vya mafunzo ya kurekebisha tabia badala ya watu wanaotoka magerezani wanaingia mitaani wakiwa wamejifunza mbinu za uhalifu badala ya tabia nzuri.
Wafungwa wanaomaliza vifungu vyoa hasa vijana wamekuwa wakitoka magereza wakiwa wameharibikiwa zaidi kuliko hapo awali wengi wakiwa ni wavuta bangi hali ambayo inawafanya kujiingiza katika uhalifu na kurejea tena kutumikia vifungo.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home