Mzee wa tafakari

Tuesday, January 23, 2007

HakiElimu imeadhibiwa kwa kusema ukweli


WIKI hii serikali lifanya maamuzi mazito ya kulipiga marufuku shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu kuchapisha taarifa au ripoti zinazohusiana na shule za Tanzania.

Uamuzi wa serikali upo katika waraka wake ambao unalipiga shirika hilo kufanya utafiti na kutoa vitabu na machapisho yoyote katika shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.

Sababu ambayo serikali imetoa kwa kulipiga marufuku shirika hilo ni kuwa limekuwa likitoa matangazo ya kudhalilisha serikali kwa kubeza mafanikio ya elimu yaliyopatikana na kwamba hatua hiyo inatoa picha mbaya kwa wananchi.

Moja ya matangazo hayo yanaonekana yanaiudhi ni lile linalotolewa katika redio na televisheni likieleza jinsi baadhi ya wakuu wa shule wanavyotumia vibaya fedha za Mpango wa Elimu kwa Shule za Msingi nchini (MMEM).

Sababu nyingine ambayo imetajwa na serikali ni kushindwa HakiElimu kufuata mwongozo iliyopewa na wizara ya Elimu na Utamaduni licha ya kuonywa mara kwa mara.

Kwa hakika, uamuzi huu unasikitisha kwa sababu hakuna mpenda maendeleo yoyote ambaye anaweza kuchekelea uamuzi huu hata kidogo.

Nasema kwa mpenda maendeleo hauwezi kumfurahisha kwa sababu ni dhahiri unaziba mwanya wa upashanaji habari na uimarishaji wa mijadala ya kidemokrasia.

Hivi kweli yanayosemwa katika matangazo ya Hakielimu hayapo hapa nchini? Ni swali ambalo tunajiuliza.

Tunajua kuwa kuna maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika sekta ya elimu nchini na serikali ya awamu ya tatu, lakini pia lazima tukiri pia kuna upungufu upo ambao unaweza kuwa kikwazo cha kufikia mafanikio makubwa zaidi. Upungufu huu unaweza kuwa unachangiwa baadhi ya watendaji katika Wizara ya Elimu na Utamaduni.

Wizara ya Elimu na Utamaduni ambayo inajukumu la kusimamia elimu nchini, ina wajibu pia wa kuangalia na kufuatilia yanayosemwa na vyombo vingine badala ya kuchukua uamuzi wa kuvifunga mdomo.

Dalili za kutaka kuifunga HakiElimu mdomo zilianza kujionyesha siku nyingi baada ya Waizri wa wizara hiyo, Joseph Mungai kulalamika kuwa matangazo yanayotolewa na shirika hilo yanamwudhi kwa vile yanabeza mafanikio yaliyopatikana.

Mimi naamini kuwa uamuzi wa kuifunga mdomo Hakielimu ambao manadalizi yake yalianza siku nyingi, umechukuliwa kwa sababu nyingine na sio hizo za zinazotajwa katika waraka.

Nasema sio hizo kwa sababu, kama suala la baadhi ya wakuu wa shule kutumia fedha za elimu bila ya kufuata utaratibu lipo na baadhi yake wamefunguliwa mashtaka, kwa nini serikali leo iseme ni uongo!

Tatizo la baadhi ya walimu kushindwa kufuata taratibu za ufundishaji bora nalo lipo na limekuwa likizungumza mara kwa mara hata na Mungai mwenyewe, sasa kitu gani kilichopikwa na HakiElimu?

Hakuna shaka kwamba HakiElimu ni mdau wa elimu Tanzania inaweza kuchagia mawazo, kushiriki katika kutoa michango, kuamsha mawazo mapya na kutoa changamoto zinazokwenda na mahitaji ya kizazi cha sasa katika nchi hii.

Tunashawishika kama nilivyosema hapo awali kuwa uamuzi huu umechukuliwa na serikali huenda kwa ajili ya joto la uchaguzi na sio kwa sababu kuwa kinachosema na HakiElimu hakipo.

Hata hivyo, Mungai anapaswa kuelewa kuwa matangazo ya HakiElimu hayawezi kuwashawishi wapigakura kubadilisha mawazo yao kutompigia kura chama au mgombea wanayemtaka.

Hatua ya kupiga ya serikali marufuku HakiElimu ni jambo ambalo limezua mjadala mzito kuwa huenda sasa serikali imeamua kufunga uhuru wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanaonekana kupata umaarufu kama ilivyowahi kufanya kwa Barala la Wananke Tanzania (BAWATA).

Kwa nchi inayofuata utawala wa sheria, inayoheshimu mgawanyo wa madaraka na dhana nzima ya kudhibitiana katika utendaji, ni jambo lisilokubalika kwa Wizara ya Elimu na Utamaduni kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, hakimu na wakati huo huo kuwa magereza.

Utaratibu wa namna hiyo hauruhusu haki kutendeka hata kidogo.

Ni vizuri serikali na vyombo vyake vyote vikafahamu kwamba hizi ni enzi za uwazi katika kushirikishwa wadau katika mambo yote yanaowahusu maendeleo ya wananchi.

Serikali kuendesha kila kitu itakavyo bila kutafuta na kuzingatia maoni ya wale walioko nje ya mfumo wa serikali ni kufuata utawala usio wa sheria.

Kama nilivyosema awali HakiElimu wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu yale yanayotendeka katika mashule wala hawako kwa ajili kuipaka matope serikali.

Mungai anataka kuwalazimisha watanzania kuimba wimbo wa kusifia tu mafanikio yaliyopatikana wakati tunaona yamezingirwa na baadhi ya matatizo ambayo yakiondoka, maendeleo hayo yanaweza kuonekana kwa urahisi na watu wengi.

Kinachoonekana hapa ni kuwa HakiElimu ni mtoto ambaye ameadhibitiwa sababu tu kamwona baba yake yuko uchi na akamwambia baba uko uchi jifunike.

Ina maana gani kama utamwacha baba akiwa uchi usimwambie halafu watu wote mtaa mzima wakamwona!

0 Comments:

Post a Comment

<< Home