Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Wizara ya afya mnataka madaktari, lakini wa Dk Masau hamwataki!


WIKI hii tulishuhudia mvutano wa muda mrefu kati ya mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Tanzania (THI), Dk Ferdinand Masau na wizara ya afya na ustawi wa jamii ukiendelea.

Mvutano huo ambao umechukua muda mrefu wiki hii ulichukua sura nyingine baada ya Dk Masau kuilalamikia serikali kuwa inamkwamisha kuwaleta watalaam kutoka Uingereza kutoa huduma kwa zaidi ya watoto 200 wanaokabiliwa na maradhi ya moyo nchini.

Dk Masau anasema mengi kuhusu wizara kumwekea mizengwe, lakini kubwa anasema ni wizara imekalia maombi yake ya mwaka jana kuomba idhini timu ya wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Oxford/Hospitali ya John Redcliffe kuja nchini kutoa huduma hiyo kwa wiki mbili.

Imeelezwa kwamba kama ziara hiyo ingefanikiwa, watoto 200 wangechunguzwa na 30 kufanyiwa upasuaji na kwamba gharama hizo zilitarajiwa kutolewa na Wizara ya Afrika ya Uingereza.

Dk. Masau alipasua jipu hilo wakati mke wa rais Mama Salma Kikwete alipotembelea taasisi hiyo na kumwomba mke huyo wa rais amfikishie kilio chake kwa mkuu wa nchi.

Katika barua yake aliyoiandikia wizara, inaeleza bayana nia ya taasisi hiyo kuomba serikali iiunge mkono kwani mradi huu utaendelea kuokoa maisha ya watoto wengi wa Tanzania wanaougua ugonjwa wa moyo.

Dk Masau anasema kuwa watalaam kutoka hospitali hiyo ya Uingereza mbali ya kukubali kuja nchini pia walimwandikia barua Waziri wa Afya Profesa David Mwakyusa kuomba kukubali kuingia nchini kufanya kazi.

Kwa upande Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Aisha Kigoda alisema anakumbuka jambo hili kuwa ni la muda mrefu kuanzia taasisi hiyo ilipokuwa na ofisi zake eneo la Mikocheni, ila haamini kuwa kweli kama Dk. Masau hajajibiwa.

Naye Mkurugenzi wa masuala ya Tiba Dk Zacharia Berege alisema Taasisi ya Moyo ilishafanyiwa tathini na wataalamu na anaamini kuwa Dk Masau anayo majibu ya timu hiyo.

Hatukatai inawezekana kabisa kwamba serikali inao utaratibu wake wa kushughulikia masuala nyeti kama haya hasa linapokuja suala la kuzihusisha nchi na nchi huku yakipitia katika taasisi binafsi, hilo hatuna shaka nalo.

Lakini suala hilo la kuleta watalaam kwa ajili ya kutoa tiba ya moyo hapa nchini hata kama limeletwa na mtu ambaye hafai lilipaswa kukubaliwa na serikali kulichunguza badala ya kubaki kimya.

Ninajua kuwa mvutano huo kati ya Dk Masau na wizara inawezekana unatokana na sababu binafsi na sio za kimaadili kama ambavyo imekuwa ikielezwa na wizarana watendaji wake.

Labda tu kwanza nieleze kuwea sipo hapa kumtetea Dk Masau, lakini kama nia yake ni kueleta watalaa ambao watasaidia kutoa matibabu kwa watanzania kuna ubaya gani wakikubaliwa?

Kitendo cha serikali kukaa kimya kuhusu ombi la kuingiza madaktari hapa nchini ni la kushangaza kwa sababu kwa wakati serikali imetangaza kwamba hivi sasa ina mpango wa kuingiza madaktari kutoka Urusi, China, Misri na Cuba hivi karibuni ili kukabiliana na uhaba wa uliopo inashangaza tunashindwa kuchangamkia nafasi kama hii aliyoileta Dk Masau.

Inavyoonekana wizara ya afya bado kuna matatizo makubwa ambayo yanafanya baadhi ya watu kutumia madaraka yao kukwamisha mambo ya maendeleo kwa matakwa yao.

Leo hebu wizara ya afya watuambaie ni kasi gani cha fedha wanatumia kupeleka watanzanzia wenye matatizo ya moyo kutibiwa nje ya nchi.

Zipo taarifa kwamba safari hizi za kupeleka wagonjwa wa moto nje ya nchi zimekuwa ni miradi ya baadhi ya watendaji ndani ya wizara ya afya, hali ambayo inawafanya wasikubali kuwa tiba ya moyo inaweza kufanyika hapa nchini.

Kama jambo hili ni kweli kukubali watanzania wafe kwa sababu tu ya watu wachache waendelee kupata maslahi yao ni hatari kubwa. Kila nchi hivi sasa inajitahidi kuwapatia watu wake uwezo wa kufanya mambo makubwa ndani ya nchi zao.

Kwa mfano kama tutakuwa na watalaam wa kuweza kutoa huduma bora za matatibu hapa nchini tutaweza kuokoa hela nyingi ambazo hivi sasa zinatumiwa na serikali kupeleka viongozi na watu wengine kutibiwa nje ya nchi.

Ukimya wa miezi saba unaodaiwa na Dk Masau unatoa mwanya wa kutolewa kwa tafsiri nyingi hasi dhidi ya Serikali bila ya sababu zozote za msingi, hasa ikizingatiwa kwamba idadi ya watoto wanaoteseka au kupoteza maisha wazazi wao wakitafuta huduma hiyo inaongozeka huku wengi wao wakiwa hawana uwezo wa kumudu gharama zake ambazo ni za juu mno kwa mtu wa kawaida.

Waziri Mwakyusa anapaswa kutumia busara kuliangalia suala hilo kwa macho mawili, hasa kwa kuwalenga watoto ambao baadhi yao wameorodheshwa katika ofisi zake wakisubiri kupelekwa nje ya nchi pasi na kujua siku wala saa ya kupata nafasi hiyo.

Pia waziri Mwakuyusa ambaye kitaluma ni daktari anapaswa pia kuangalia ndani ya wizara yake kuona utendaji wa maafisa wake inawezekana kabisa anapewa taarifa potofu kuhusu Dk Masau na tasisi yake kwa sababu wanatofautiana naye au waliwahi kugomba naye walipokuwa wote wizara hiyo.

Kinachoshangaza ni kwamba wizara katika shughulikia suala hili hata kama ilikuona kuwa kulikuwa na kasoro fulani katika kuingiza watalaam wake, ingetoa hata masharti fulani, lakini kukaa kimya moja kwa moja ni kuonyesha msimamo wake kuwa haitaki kile alichoomba DK Masau.

Ninapenda kutoa ushauri kwa watendaji wa wizara hii kubadilika ili waende kuligana na mazingira, lakini wainashi kwa kuangalia alama za nyakati kwani kuendelea kung'ang'ania mambo haya ubifsi ni kuliua taifa.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home