Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Kufugiwa Hakielimu ni mwanzo wa watanzania kuzibwa midomo


HATUA ya serikali kufungia tena matangazo na machapisho yanayotolewa na Shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu, inanikumbusha hadithi moja ya zamani ya Mfalme Sifa.

Hadithi hii ilikuwa ikimweleza Mfalme Sifa ambaye siku zote wananchi wake alitaka wamsifie kwa kila jambo analofanya.

Mfalme Sifa ilifikia mahali hata pale alipotoa adhabu mbaya kwa wananchi kutokana na kutawala kwa mkono wa chuma, wananchi walimshangilia.

Kuna siku alitoa adhabu ya kuawa kwa mwananchi mmoja ambaye alipatikana na hatia ya kukosoa utawala kwenye mkutano wake wa hadhara.

Siku ya kutekelezwa kwa adhabu hiyo wananchi walitakiwa kuhudhuria kushudia mwezao akichinjwa. Wananchi kama kawaida yao kwa kuogopa kumwudhi Mfalme Sifa walihudhuria kwa wingi.

Alipoaanza kuchinjwa mwananchi huyo na wapambe wa Mfalme Sifa, umati mzima ulikuwa kimya na wengine wakibubjikwa na machozi, lakini mflame alipoona hashangiliwa kama ilivyokuwa kawaida yake, alihamaki na kuangalia pande zote za umati huo akishiria anataka washangilie.

Wananchi hao kwa kuhofia nao kuingia katika mikono ya Mfalme Sifa aliwaanza kushangilia kuchinjwa kwa mwezao huku wakibubujikwa na machozi ya uchungu.

Simulizi hii kama nilivyosema awali ninaifananisha na maamuzi ya serikali ya kufungia matangazao na machapisho ya Hakielimu ambayo yanaikosoa serikali.

Nasema sema naifananisha simulizi hii na kisa cha kufungiwa Hakielimu kwa sababu, kazi ambayo inafanywa na shirika hilo lisilokuwa la kiserikali ni kutoa ushauri pale ambapo serikali imejisahau kuparekebisha.

Mvutano wa serikali na Hakielimu ulianza Agosti mwaka juzi wakati iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni ilipoizuia kutoa machapisho na matangazo yake kwa kile ilichokieleza kwamba yanaidhalilisha elimu na kisha Rais wa awamu ya tatu alikazia amri hiyo.

Kama ilivyokuwa katika agizo la kwanza, wadau, taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na hata wananchi wa kawaida wameushutumu uamuzi huo huku wakiipongeza HakiElimu kwa jitihada zake kusaidia kuinua sekta hiyo adhimu.

Ni kutokana na mchango mkubwa wa shirika hilo ndio maana baadhi ya mambo ambayo yanakosolewa katika matangazo ya Hakielimu yamefanyiwa kazi na serikali.

Baadhi ya kero ambazo zimefanyiwa kazi na serikali baada ya kutolewa hadharani kupitia matangazo na Hakielimu ni kero ya mishahara ya walimu.

Hivi sasa walimu wanapata mishahara tarehe 25 ya kila mwezi, hali ambayo imewasaidia kuwapa ahueni ingwa mishahara yao bado haikidhi gharama za maisha.

Shirika hili kwa uungawa kabisa baada ya kuona kuwa serikali imeondoa kero hiyo liliamua kuondo matangazo yake yaliyokuwa yakizungumzia ucheleweshaji wa mishahara kwa walimu.

Tangazo lingine ambalo Hakielimu ilikuwa ikilizungumzia kwa muda mrefu ni kero ya kuchapwa viboko shule ambayo sasa serikali imeamua kulifanyia kazi.

Wazi kuwa mchango wa Hakielimu katika kusaidia kuikumbusha serikali baadhi ya majukumu yake ni mkubwa hautakiwi kubezwa hata kidogo.

Si kweli hata kidogo kuwa kila tangazo au chapisho litolewalo na HakiElimu lina lengo la kuvuruga au kupotesha mikakati ya uboreshaji wa elimu nchini.

Matangazo ya Hakielimu yamekuwa yakichangiza maslahi bora na mazuri kwa walimu na elimu kwa ujumla. Imetumia maigizo halisi ya dhiki ya walimu hadi serikali ikajirekebisha.

Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kwamba serikali yetu inayoheshimu uhuru wa kujieleza na kutoa maoni itakuwa haipendi kukosolewa hasa ikiwa kama aina yenyewe ya kukosolewa ni hiyo.

Kama serikali haitapenda kukosolewa basi huenda sasa viongozi wake wanataka kuishi kama maisha ya Mflame Sifa ambaye alitaka kusifiwa tu kwa kila jambo alilokuwa akitaka kulifanya.

Naamini uamuzi wa kulifungia Hakielimu ulichukuliwa bila ya Rais Jakaya Kikwete kushirikishwa, hivyo ninaamini kabisa kama alivyoahidi alipokutana na waandishi wa habari wiki hii kuwa alitachunguza na kulitolea maamuzi.

Hakuna nchi duniani ambayo inaweza kupata maendeleo ya kweli kama wananchi wake wamezibwa midomo ili wasikosoe serikali.

Kama rais Kikwete ataridhia kupigialia msumari wa mwisho kwenye jeneza la kuizika Hakielimu, basi huo utakuwa ni mwanzo wa kuwafanya watanzania sasa wawe watazamaji tu katika matatizo yote yaliyopo.

Lakini ieleweka kwamba ingawa serikali ya awamu ya nne imeaanza vyema kwa viongozi wake kupendwa, lakini wajue kwamba kuna mambo ambayo wanapaswa kukosolewa.

Ukisoma historia ya utawala madkiteta duniani inaanzia katika kuzuia uhuru wa kujieleza na baadaye kuingia katika mambo makubwa.

Sisi Tanzania hatutaki kufikia huko au alikofikia Mfalme Sifa ambaye alitaka kusifiwa kwa kila ajmabo alilolifanya hata kama hali maslahi kwa nchi.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home