Mzigo wa kodi katika mishahara ni mauaji kwa wafanyakazi
SERIKALI wiki hii ilitangaza viwango vipya vya mishahara
ya watumishi wake ili kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akihutubia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kuwa ataboresha maisha ya wafanyakazi wake kwa kupandishia mishahara.
Viwango vipya kwa mujibu wa waziri wa nchi ofisi ya Rais utumishi, Hawa Ghasia alivyotangaza bungeni, vimepanda kati ya asilimia 15.9 hadi asilimia 50 ya mishahara ya sasa.
Kwa maana nyingine ni kuwa mshahara wa sasa wa kima cha chini cha serikali cha sh 65,000 kwa mwezi umepanda hadi sh zaidi ya 100,000 kwa mwezi.
Katika tangazo lake ambalo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu na watumishi wengi wa umma, serikali haikutaja kima cha chini cha mshahara wake ambacho kitalipwa kuanzia mwezi huu kitakuwa kiasi gani ila imetaja asilimia tu.
Hata hivyo, Waziri Ghasia, alisema kutokana na maelekezo ya sera viwango vya mishahara kwa watumishi ambao watapandishiwa zaidi ni wataalam wa fani zote na watumishi walio katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa kauli hiyo polisi, wanajeshi, usalama wa taifa, madaktari na wataalam wengine ndio watafaidi kwa kiasi kikubwa na kapu hilo la mishahara na kuwaacha watumishi wengine waliotajwa na waziri kuwa ni wale wa kawaida wakiendelea kujikongoja kwa kulipwa kidogo.
Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo wa serikali kutoa nyongeza katika mishahara wa watumishi wake lakini fedha nyingi ilizoziongeza zitairudia nyenyewe kutokana na kuwapo kwa kodi nyingi mno katika mishahara.
Ukiachia watu wa kima cha chini ambao baadhi yao huwa hawakatwi kodi, lakini watumishi wenye mishahara mikubwa sehemu kubwa ya mishahara yao itachukuliwa tena na serikali kama kodi.
Watu wengi wamekuwa wakihoji wakiwamo baadhi ya wabunge kwa nini serikali imebebeshe mzigo mkubwa kiasi hicho cha kodi wafanyakazi wakati inaweza kupanua wigo wa kukusanya kodi katika maeneo mengine?
Yapo baadhi ya maneno ambayo tuanaamini kabisa hayajaguswa katika ukusanyaji wa kodi. Kwa mfano pamoja na kupata zaidi ya sh 200,000 kwa wiki kw waongoza sherehe maarufu MC lakini hakuna mpaka sasa utaratibu uliowekwa wa watu hao kukatwa kodi.
Kama hiyo haitoshi pia wapigapicha za video za mitaani ambao imedhihirika wanajipatia zaidi ya sh 500,000 kwa wiki lakini hakuna mtu ambaye anawafuata ili nao walipe kodi ya mapato.
Wamiliki wa nyumba nyingi nchini wananaokodisha kwa wapangaji nao hawalipi kodi ya mapato. wapo watu wanaomiliki zaidi ya nyumba 10 wanazolipwa zaidi ya sh 100,000 kwa mwezi lakini hawalipi kodi.
Kuna nyumba ngapi masalani jijini Dar es Salaam ambazo zinapangishwa? ni wazi kuwa zipi nyingi mno. Serikali inapoteza mapato kiasi gani kutoka kwa watu hawa kama ingeamua kuogeza wingo wake wa ukusanyaji wa mapato? Nadhani bado serikali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hazaijafanya kazi ya kutosha.
Kwa ujumla kuna biashasra nyingi ambazo zinawapatia mapato makubwa baadhi ya watanzania bado hazijaangaliwa kwa ajili ya kushirikishwa katika kukwa kodi ya mapato, lakini wafanyakazi ndio ambao wanaongezewa kodi kila siku kwa vile tu ni rahisi kuzipata fedha zao.
Wakati serikali ikijitahidi kuongeza makusanyo ya kodi kwa kuendelea kukamua vyanzo vile vile vya mapato wakiwamo wafanyakazi ambao ndio waathirika wakubwa, baadhi ya wafanyabaishara wakubwa hawalipi kodi.
Hivi sasa sio jambo la siri kuwa wafanyabiashara hao kutokana na utaratibu wetu kuwa mbovu mipakani wanaingiza bidhaa nyingi za mabilioni ya shilingi bila ya kuzilipia ushuru.
Ushahidi wa jambo hili unaojionyesha wazi katika maeneo yaliyopo karibu na mipaka jinsi ambavyo yamebadilika kuwa njia za kuingizia bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru.
Kwa mfano eneo la Maramba mkoani Tanga hivi sasa ndilo linaloingiza bidhaa nyingi kutoka Kenya kuliko hata kwenye mpaka wenyewe wa Horohoro. Hii inaonyesha dhahiri kuwa serikali inapoteza mabilioni ya shilingi ya ushuru wa forodha kutokana na kushidwa kuthibiti njia hizo za panya.
Wakati hayo yakiendelea katika eneo la Maramba, hata ufukwe wa bahari ya Bagamoyo nao umegeuka kuwa bandari ya majahazi kuingizi bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru kutoka nje.
Ninapotafakari, ninadhani kuwa kuna haja sasa serikali iache kukamua tu vyanzo vile vile vya mapato badala yake itafute vyanzo vipya ili iweze kuongeza mapato yake ikiwamo kuziba njia za panya mipakani.
Mbali ya kuongeza vyanzo vipya vya mapato pia serikali inapaswa kubana matumizi ya watumishi wake ili fedha hizo zifanyie shughuli nyingine za maendeleo.
Hivi sasa serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya masurufu ya safari kwa watumishi wake hali ambayo inaonyesha wazi ni matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika bajeti ya utumishi ya mwaka huu inaonyesha kuwa zimetengwa fedha nyingi kwa ajili ya posho za safari badala ya kuwatengea watumishi wengi mishahara.
Ni kutokana na hali hiyo ya utumishi serikali kuwa katika matatizo makubwa yakiwamo ya kupata mishahara midogo ambayo imeelemewa na makato mengi ndio maana vijana wengi hivi sasa hawana hamu kuajiriwa.
Wakati kijana ambaye ni mhasibu mwenye shahada ya juu ya uhasibu serikalini anapata mshahara mdogo mno ambao ni sawa na anaopata tarishi TRA, mtu mwenye taaluma kama yeke aliyepo katika kampuni ya umma au binafsi anapata kuanzia sh 2,000,000 kwa mwezi hali ambayo inakatisha tamaa kajiriwa serikalini.
Kumpa mshahara mdogo mtumishi wa serikali ni kuminya pensheni nzuri ambayo ataipata wakati anapostaafu. Hivi sasa watu wengi wanalazimika hata kusema uongo kuhusu umri wao ili wasistaafu mapema kwa vile pensheni watakayopata baada ya kustaafu itaisha baada ya mwaka mmoja tu na kuwafanya wafe haraka.
Hivi karibuni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), lilipendekeza kuwa ili wafanyakazi wa kitanzania serikalini waweze kuishi maisha bora kama watu wengine kima cha chini kinatakiwa kuwa sh 300,000 kwa mwezi.
Nadhani mapendekezo hayo ni mwafaka lakini labda yasiwekatwe kodi kubwa ya mishahara iliyopo hivi sasa. Kwa msahahara huo utakatwa kodi iliyopo hivi sasa ni wazi kuwa kisi kikubwa kitarejea kwenye mikono ya serikali tena na kumcha mfanyakazi hana kitu tena.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home