Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Ripoti Maalum

Makambi ya wavuvi ziwa victoria: Mtambo wa kuzalishia ukimwi
*Ngono zinafanyika ovyo mitaani
*Wauza duka wageuka madaktari
*Hela za wavuvi zinashawishi wanawake kuingia visiwani

STAREHE kubwa ambavyo mtu huiwaza kuifanya baada ya kumaliza kazi za uvuvi au shughuli nyingine katika visiwa vinavyotumiwa na wavuvi kuvulia samaki katika Ziwa victoria ni kufanya ngono na kunywa pombe.

Ni jambo la kawaida kabisa kumwona mvuvi akirejea kisiwa kutoka ziwani, mtumwi wake unapotia nanga na kumaliza kuuza samaki wake, akiulizia kama kuna mwanamke mgeni aliyeingia kisiwani ili amfutilie kumwomba wafanya naye ngono.

Ni kawaida pia kwa wanaume wa visiwa hivi kushindana kumpata mwanamke mgeni anayeingia wakidai kwamba waliopo walishashoka nao.

Mwanamke katika visiwa hivi ni mali adimu kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya wanaume kuliko wanawake.

Katika visiwani hivi falsafa kubwa inayotawala ni mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama kwa mana ya kwamba kama huna pesa huwezi kupata mwanamke.

Wengi wa wanawake hawa wanaofanyabiashara ya ukahaba, huhama kutoka kisiwa kimoja hadi kingine, wapoona wameanza kuchokwa na wateja au inapotokea wanasabisha ugomvi wa kumgombewa na wanaume.

Bei ya chumba cha kulala wageni katika visiwa vingi ni kati ya sh 500 hadi sh 1,000 kwa chumba kwa kukodi siku nzima. Kwa mfano katika kisiwa cha Mchangani chumba kimoja cha kulala ni sh 1,000.

Ili kuondoa migogoro ya kugombea wanawake baadhi ya visiwa vimeweka sheria ambayo ina mlinda mwanamke dhidi ya manyanyaso dhidi ya wanaume kwa kuruhusu wapenzi hao kuwekeana mikataba ya hela ambazo atalipwa mwanamke na muda watakaokuwa pamoja.

Hata hivyo, mikataba hiyo imekuwa ikivunjwa baada ya mwanamme anapo kwenda kulala ziwani nyuma, mwanamke hupata mtu mwingine. Kwa wastani katika visiwa vyenye watu wengi wanawake wanafanya ngono zaidi ya wanaume kwa siku.

Swali kubwa la kujiuliza ni je wanatumia njia salama ya kufanya mapenzi kwa kutumia kondomu?

Mmoja wanawake waliopo katika kisiwa cha Mchangani chenye wastani wa wakazi 10,000, kilichopo katika wilaya ya Sengerema, Stella Leshe anasema ni mara chache sana kuona mwanaume anayefanya na mapenzi anatumia kondomu.

Anasema wanaume wanafanya shughuli za uvuvi hawataki kutumia kondomu wanasema wanapotumia fedha zao wanalizomlipa mwanamke hawawezi kuzifaidi.

Stella ambaye anatoka mkoa wa Mara anasema ameingia katika kisiwa hicho kuuza baa baada ya kufiwa na mume wake ambaye walikuwa wakiishi wote mjini Musoma mwaka juzi.

Anasema baada ya kukosa mtu wa kuwatunza watoto wao wanne ambao wamezaa na mume wake aliamua kumfuata rafiki wake ambaye alikuwa anafanya kazi ya kupika chakula katika kisiwa cha Juma lakini baadaye aliamua kuingia katika kisiwa hiki kuuza baa.

Anasema ingawa hapati mshahara mkubwa kutokana na kuuza baa lakini anapata hela ya kulisha watoto wake Musoma kutokana na hela ambazo anahongwa na wanaume.

"Ni kweli nalazimika kufanya mapenzi na wanaume wengi ili niweze kupata fedha za kutunza watoto wangu ambao wa kwanza anasoma darasa la tano, tatu na darasa la kwanza.

Kwa mujibu wa wasimamizi wa gesti zilizopo katika visiwa hivi wengi wanasema kuwa wakipata wateja wanaotoka mijini kununua samaki au wengine wakitoka kama wamelala na wanawake hukuta kuna kondomu zimeaachwa ingawa hazijatumika.

Lakini kwa wakazi wa visiwa hivyo ambao wengi wao ni wavuvi, hali ni tofauti kabisa hakuna kondomu yoyote ambayo huonekana chumbani baada ya watu kutoka kufanya ngono.

Msichana Pendo Samson (24) msiamizi wa gesti mojawapo katika kisiwa cha Mchangani anasema ni nadra sana kukuta chumba kimeaachwa kondomu iliyotumika ambacho kimetumiwa na watu walioingia kufanya ngono.

Baadhi ya wanaume katika kisiwa cha Mchangani wanasema kutumia kondomu inawafanya eachelewa kumaliza tendo la ngono na kwamba hata raha yake ni ndogo.

Ingawa ni eneo dogo lenye mita 500 linalokaliwa na watu kandokando ya ufukwe wa ziwa na nyumba nyingi zaidi ya 200 ndogo ndogo zilizojengwa kwa kutumia mabanzi ya miti kuanzia chini mpaka juu, lakini wakazi wake muda wote wapo katika pilika pilika nyingi muda wote.

Wakati wengine wanaingia katika mitumbwi kwenda kuvua samaki, wengine ndio wanaingia baa kutumia hela zao na kutafuta wanawake kwa ajili ya kufanya ngono.

Hali hii ya kufanya ngono isiyosalama kwa wakazi wa visiwa hivi mbali ya kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa ukimwi pia ndiyo ambayo inawafanya wengi kuambukizwa magonjwa wa zinaa kama gono na kawende.

Wanaume wengi wa visiwa hivi kutokana na kuwapo kwa wanawake wachache mara nyingi mwanamke sio wa mtu mmoja, anaweza kuchukuliwa na mtu yoyote ili mradi awe na uwezo wa kumpa hela na kumlisha.

Kwa mfano mvuvi akienda kulala ziwani kuvua samaki kama ana mwanamke ambaye alikuwa naye mchana wanastarehe akiondoka tu, anachukuliwa na mwingine mwenye uwezo.

Kutokana na wanawake kufanya mapenzi na wanaume wengi wamekuwa wakipata na kusambaza magonjwa ya zinaa kwa urahisi zaidi kwa karibu watu wote wanaishi katika visiwa hivi.

Wanaopata ungonjwa huu wanapata wapi tiba ukichukuliwa kuwa eneo hilo halisi huduma za afya ya aina yoyote?

Muuza duka la dawa mmoja aliyepo katika Kisiwa cha Mchangani John (sio jina lake halisi) anasema dawa za tetecyline ambazo zinatumika kutibu magonjwa wa zinaa ambazo zipo katika duka lake zina wateja wengi sana.

Pia dawa za kutibu ugonjwa wa fangas za kupaka na za vidonge, zinanunuliwa zaidi na wateja wake kutokana na watu wengi kusumbuliwa na ugonjwa huo.

Anasema ingawa hawana utalaam wa kusomea kuhusu dawa lakini kutokana na uzoefu alioupata wa kuuza dawa hizo kwa muda mrefu anaweza hivi sasa hata kumsikiliza mgonjwa na kumshauri aina ya dawa ya kutumia.

John anasema mbali kupata wateja wengi wanaougua magonjwa wa zinaa lakini pia hupata watu wanajisikia kuugua malaria na kuwashauri aina ya dawa ya kutumia.

Anakiri kuwa ni vigumu kujua aina ya ugonjwa anaugua mtu, lakini kutokana na watu kumlazimisha awapatia dawa za kutibu ugonjwa wao, anafanya hivyo sababu kwa kuuza dawa kisiwani humo anaonekana kuwa ndiye mtalaam wa magonjwa.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa utumiaji wa dawa holela bila ya kufuata taratibu kwa wakazi wa visiwa hivi pia ni moja ya sababu ya watu kutahirika na wengine kupoteza maisha yao.

Hata hivi sasa kutokana na dawa za dukani kuonyesha kutowasaidia wengi kupona ugonjwa wao hasa wa ngono na kaswende hivi sasa wanatumia dawa za mitishamba ambazo zinauzwa na wamasai kutoka mkoani Arusha.

Wamasai wamegundua kuwa dawa hizo zina soko kubwa kutokana na watuywengi kuwa na ugonjwa wa zinaa kutokana na kufanya ngono zisizo salama.

Mmoja wa masai hao ambaye yupo katika kisiwa cha Mchangani, maarufu kwa jina la Ole Masai anasema anatembeza dawa za ke kwa kutumia baskeli ili kuwapa kwa urahisi wateja wake.

Anasema anauza dawa za maji kwa ajili ya kutibu gono na kaswende, kuongeza nguvu za kiume, malaria na za wanawake kwa ajili ya kuweka katika sehemu za siri ili wanaume wajisikie raha wakati wakifanya nao mapenzi.

"Nauza dawa za aina zote kuanzia za magonjwa wa zinaa, mapenzi inayoitwa lukomolo (limbwata) na zile za kuongeza nguvu kwa wanaume," anasema Ole Masai.

Anasema hata hivyo dawa ambavyo inapendwa zaidi na wateja wake ni ya lukumolo kwa wanawake ambayo wanaitumia kuwafurahisha zaidi wanaume ili wapatiwe hela nyingi na ile ya kutibu gono ambayo ipo katika majimaji.

Mmasai huyo anasema anatembea na dumu la lita tano la dawa hiyo ya kutibu magonjwa ya zinaa pamoja na kikombe ili kuwapa muda wowote anapokutana na mtu ambaye ana tatizo hilo.

Kwa hakika mmasai huyo ni maarufu kweli kweli katika kisiwa hiki, huwezi kutembea mita mbili bila ya kusikia watu wakimwulizia iwe wanawake au wanaume wakiwa na matatizo mbalimbali.

Ilikuwaje akafika katika visiwa hivi kutoka Arusha? Ole anasema alisikia taarifa za kuwapo kwa visiwa hivi na mahitaji ya dawa alizonazo siku nyingi hivyo akaamua kuingia mkoani Mwanza na baadaye kuingia katika visiwa hivi.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa dawa hizo wanazotumia kwa ajili ya kutibu magonjwa wa zinaa, lakini kasi ya maambukizi ya ukimwi katika visiwa hivi ni makubwa mno.

Ingawa hakuna vifo vingine vinavyotokana na watu kuungua hadi kufa kutokana na ugonjwa wa ukimwi, lakini mara nyingi mtu akianza kuungua na kujihisi kuwa anaumwa ukimwi huhama kwenda katika kisiwa kingne na akizidiwa huenda nyumbani kwao kufikia huko.

Hali hii huenda ndiyo ambayo inawafanya watu wengine wasiwe na hofu ya kuwapo kwa ukimwi katika visiwa hivyo kwa vile hawawaoni watu waliopo kitandani wakiungua ukimwi.

Maambukizi mengine mengi katika visiwa hivi vya wavuvi yanaongezwa na kuingia kwa wingi kwa watu waliofisiwa na wanaume au wake zao na kupata unyanyapaa katika jamii inayowazunguka, na hivyo kuamua kukimbilia huko.

Watu hao wakifika katika visiwa hivyo hufanya ngono na watu mbalimbali bila ya kujulikana kuwa wameathirika na virusi vya ugonjwa wa ukimwi.

Utafiti uliofanywa mwaka huu na shirika lisilokuwa la kiserikali la Laneso katika kisiwa cha Juma chenye idadi ya watu 5,200 kilichopo katika wilaya ya Mwanza inaonyesha kuwa wakazi wengi katika kisiwa hicho ni vijana ambao wanavua dagaa ambao wanakabiliwa na maambukizi makubwa.

Hata hivyo, juhudi za shirika hilo, hazitatosha kama wakazi wengine katika visiwa vinavyotumiwa na wavuvi katika ziwa victoria hawatapata elimu ya ukimwi, kwa vile maishja ya wavuvi huwa ni ya kuhama hama kila siku.

Afisa Misitu wa Wilaya ya Sengerema ambaye ndiye mmiliki wa visiwa vyote vilivyopo katika eneo la wilaya hiyo, Ernest Mkilindi anasema kasi ya maabukizi ya ugonjwa wa ukimwi katika visiwa hivyo vya wavuvi ni kubwa mno.

Anasema wavuvi wengi hawana elimu ya kufanya ngono salama, hali ambayo imesababisha wengi kujikuta wakiambukizwa ugonjwa wa ukimwi.

Hata hivyo, anasema sababu nyingine inayosababisha kuwapo kwa ugonjwa wa ukimwi katika visiwa hivyo, hela nyingi wanazopata wavuvi ambao kutokana na kuwa visiwani wanao njia pekee ya kuzitumia ni kufanya ngono.

Mkilindi anasema ingawa kuna baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamekuwa yakijitolewa kufika katika visiwa hivi kupima na kutoa ushauri nasaha, lakini inaonekana wavuvi na watu wengine waliopo visiwa somo la kinga halijawaingia.

Hata hivyo, ukweli ubaki kuwa hakuna hatua za makusudi ambazo zimechukuliwa na serikali katika kutoa elimu ya ukimwi kwa watu wanaoishi katika visiwa hivi ambavyo ni eneo la mistu ya taifa.

Pia kukosekana kwa mtandao wa serikali katika eneo hili na ugumu wa usafiri wa kufika ni moja ya sababu ya kukosekana mawasiliano ya viongozi wa serikali.

Juhudi za serikali kuhamasisha kuhusu suala la ukimwi bado hajaweza kuwafikia watu wanaoishi katika visiwa hivi, ingawa baadhi ya wavuvi wa visiwa hivi wanasema wanataka sana mafunzo hayo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali idadi hiyo ya watu waishio na virusi vya hivi sasa nchini imeongezeka kutoka 900,000 mwaka 1990 hadi kufikia milioni mbili.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home