Ripoti maalum
Mauaji ya kinyama Ziwa victoria
*Wavuvi wanaporwa na kuuawa
*Majambazi yanatumia silaha nzito
"Jambo lingine nitakalozungumzia hapa ni kuhusu ujambazi, ujambazi umekithiri moja kwa moja na ninashangaa ujambazi unapotokea Dar es Salaam kila mtu ndio anaanza kuzungumzia ujambazi upo.
Mimi nilishazungumzia hapa bungeni katika bunge lililopita kwamba ujambazi Buchosa ni kwamba inapofika saa 12 jioni bendera ya serikali inapoteremshwa wale watu wanajichukulia madaraka mpaka asubuhi, watu hawalali kule wananyanyaswa, wanauawa ziwani wananyang’anywa vifaa vyao vya kuvulia, samaki," hayo ni malalamiko ya Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo bungeni Julai mwaka huu wakati akielezea hali ya uharamia ziwa victoria.
Mbunge huyo anatoa mfano wa matukio hayo kuwa siku nne zilizopita akiwa katika kikoa hicho cha bunge alipewa taarifa kuwa majambazi yalivamia katika kisiwa Zilagula, Mchangani na Maisome na kunyang’anywa zaidi ya injini 20 za kuvuliwa.
Matukio anayozungumza mbunge Chitalilo ni mfano wa matukio mengi ya ujambazi anayotokea kila siku katika Ziwa victoria mengi yakiambatana na uporaji na mauaji.
Ingawa jeshi la polisi nchini limeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa ujambazi wa kutumia silaha katika maeneo mengi nchini lakini ujambazi ndani ya visiwa ziwa Victoria bado unaendelea kushika kasi.
Uvamizi huo dhidi ya wavuvi unaofanywa na majambazi unafanyika kwa kutumia silaha za kisasa kama vile bunduki aina ya SMG na bastola.
Uporaji huu unafanyika wazi wazi bila ya wahusika kuwa na wasiwasi kutokana na eneo la ziwa hususan mbali na nchi kavu kukosa udhibiti wa vyombo vya dola.
Kutokana kutokuwapo kwa mtandao wa ulinzi wa jeshi la polisi katika ziwa hususan katika visiwa vinavyotumiwa na wavuvi ndiyo maana majambazi haya yamekuwa yakipora na kupata muda wa kuwadhalilisha wanaowapora vifaa vya uvuvi kuchagua aina ya adhabu ambayo watapata kutoka kwa wahalifu hao.
Mmoja wa wavuvi anayefanyia shughuli zake katika kisiwa cha Kabiga kilichopo katika Ziwa hilo, Joshua Nyabirema anasema adhabu hizo ni 'car wash' yaani kukatwa mikono yote miwili, 'pensi' kukatwa miguu yote au 'kucheka maisha yako yote' kukatwa shavu na kubaki meno nje ua 'kukamata lami' yaani kutumbukia kwenye maji.
Anasema yeye na mwezake mwanzoni mwa mwaka huu walivamiwa na majambazi yakiwa na bunduki usiku wakati wanalinda nyavu zao usiku ziwani.
Nyabirema anasema kilichowaokoa wasiuawe na majambazi hayo ni boti ya doria ya bosi wao ambayo ilifika katika eneo walilokuwa wameweka nyavu zao na kuanza kurushiana risasi, hali iliyowafanya majambazi kukimbia katika eneo hilo kwa kasi kwa kutumia mtumbwi wao wa injini yenye nguvu kubwa.
Hata hivyo, tayari walishachukua injini yao waliyokuwa wakiitumia katika mtumbwi wao na wakati huo ndio walikuwa wameamriwa kuchagua aina ya adhabu ili wawaadhibiwe.
Hata hivyo, Mvuvi mwingine wa kisiwa cha Ikulu, Neneleja Nhomango anasema matukio mengi ya ujambazi katika ziwa victoria huwa hayafahamiki na vyombo vya dola kutokana na kutokuwapo kituo chs polisi karibu.
Anasema mara nyingi wakiwa ndani ya ziwa wanavua samaki hukutana na maiti zinazoelea majini zikionyesha kuwa na majeraha makubwa hali ambayo inaonyesha kuwa watakuwa wavamiwa na majambazi wakati wanbasafiri au kuvua samaki.
Hata hivyo, baadhi ya maiti ambazo zimekuwa zikionekana zikilea katika baadhi ya visiwa vinavyotumiwa na wavuvi katika ziwa hilo zikiwa zimekatwa baadhi ya viungo vya mwili ni ushahidi kuwa matukio hayo bado yanaedelea kwa kiasi kikubwa.
Vitendo hivyo vya ujambazi vilijidhihirisha mwezi uliopita baada ya majambazi saba kuvamia mitumbwi ya wavuvi wa Mchangani ziwani na yakaweza kukamatwa huku wawili wakiuawa kwa risasi na wavuvi hao ambao nao walikuwa na boti ya kulinda doria.
Baada ya kukamatwa majambazi hayo matano ambayo yalikuwa hai yalirejeshwa katika kisiwa cha Mchangani ambako wavuvi na watu wengine wanaoishi katika kisiwa hicho waliwachoma moto na kuwazika katika kaburi la pamoja.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya baadhi ya visiwa vinavyotumiwa na wavuvi katika Ziwa Victoria mkoni Mwanza, majambazi hao wamekuwa wakitumia mitumbwi iliyofungwa injini kubwa ambazo zinawafanya wakipora sehemu moja kukukimbia kwa haraka ili wasikamatwe na wavuvi wengine.
Inaelezwa kuwa baadhi ya majambazi haya yanatoka nchi jirani wamekuwa wakiiba na kukimbialia nchini kwao.
Mmoja wa wavuvi katika kisiwa cha Zilagula, Juma Mchele amasema ingawa wamekuwa wakienda kuvua ndani ya mitumbwi yao na mapanga na mikuki ya kusaidia kupambana na majambazi, lakini wamekuwa wakikwama kupambana nayo kwa vile yanatumia bunduki na bastola.
Akisimulia mmoja ya matukio ambayo ya ujambazi aliyowahi kukutana nayo mwezi uliipota anasema akiwa na mwezake katika mtumbwi wamelala usiku ndani ya maji walivamia na majmbazi ambayo yalifika yakiomba msaada wa mafuta, lakini mtu wao ulipokaribnia walitoa bunduki na kuwateka kisha wakachukua injini ya mtumbwi wao na kuondoka.
Mchele anasema hiyo ilikuwa bahati kwako kwani hayakushambulia kama ilivyo kawaida yao ya kupora na kuua au kujerehi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Zelothe Stephen alipoulizwa anasema atafuatilia suala hilo kwa karibu taarifa hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi(IGP) Said Mwema akiwa mkoani mwanza Novemba 26 mwaka huu, alikiri kuwa jeshi lake limeshindwa kudhibiti uharamia katika Ziwa victoria kutokana na uchakavu wa boti za polisi.
Mwema aliwaambia wadau wa ulinzi shirikishi mjini Mwanza, ambao walilalamikia kuwa hawana ulinzi polisi ziwani dhidi ya majambazi.
Anasema ni kweli jeshi langu haliwezi kudhibiti uhalifu huo ziwani kwa kiwango kizuri kwani nimeangalia hali ya boti tulizonazo ni mbaya sana, nimezungumza na watalaam kuona tunaweza kuziboresha vipi, ili zilizopo zianze hata kuzunguka ziwani, lakini hilo pia linahitaji fedha.
Mwema anasema suluhisho la matatizo yote katika ziwa victoria dhidi ya uhalifu ni kuomba bajeti itakayotoa uwezo kwa jeshi hilo kununua boti mpya za kisasa.
Mmoja wa wadau wa uvuvi wa samaki mjini Mwanza Paul Malima, anasema ingawa jeshi la polisi limefanikiwa kudhibiti kwa kiwango kikubwa majambazi nchi kavu hali bado ni mbaya kwa upande wa eneo la ziwa Victoria.
Anasema wavuvi wamekuwa wakiuawa na kuporwa ama nyavu, samaki au injini zao za mitumbwi na wahalifu ambao mbali ya kuwanyang'anya vifaa vyao za uvuvi wamekuwa wakifanyia vitendo vya kinayam vya kuwakata viungo vya mwili kikatili vinavyowasababishia vifo.
Kutokana kufanyiwa unyama huo, wavuvi wamekuwa wakitoa mali zao bila ya ubishi na hivyo kuwafanya wabaki masikini na kushindwa kuchangia pato la serikali.
Afisa Mistu wa wilaya ya Sengerema ambaye ndiye msimamizi mkuu wa visiwa ambavyo ni hifadhi ya taifa vilivyopo katika wilaya yake, Ernest Mkilindi anakiri kuwa hali ya usalama katika visiwa hivyo sio ya kuridhisha.
Anasema anapofanya safari ya kukagua visiwa hivyo , hulazimika kuambatana na askari polisi kwa ajili ya kumlinda dhidi ya majambazi wanaolipo katika maeneo ya ziwa.
"Kwa kweli vitendo vya ujambazi vipo, ndiyo maana nnapofanya safari za kukagua visiwa hivyo nilazimika kusindikizwa na askari polisi wenye silaha," anasema.
Wakati akilihutubia bunge mara baada ya kuapishwa kuwa rais, Desemba 30 mwaka jana Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuongeza uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ujambazi na kuzagaa kwa silaha ndogondogo ambazo zinatumika kufanyia uhalifu dhidi ya raia wema.
Mbali ya wavuvi wa samaki kukabiliwa na hatari ya kuporwa vifaa vya uvuvi na majambazi na kuuawa pia wanakabiliwa na kuliwa na mamba wanaoishi katika visiwa hivyo.
Mamba ambao hupendelea zaidi kukaa kando kando ya ziwa katika maji yenye kina kidogo wamekuwa wakiwakamata na kuwala wavuvi wanaotega samaki kwa kutumia ndoano au wale wanaokwenda kuoga ziwani.
Moja ya matukio ya hivi karibuni ya mambo kula wavuvi la mkazi wa Kijiji cha Chabula, Kata ya Kongolo wilayani Magu, Emmanuel Jummanne (34) ambaye aliliwa na mamba Desemba mwaka huu wakati akivua samaki katika Ziwa Victoria kwenye kjisiwa cha Shukla wilyani Magu mkoani Mwanza.
Kama hiyo haitoshi katika kisiwa cha Ikulu kilichopo katika wilaya ya Sengerema, jumla ya watu watatu wameliwa na mamba Novemba mwaka huu wakati wakioga.
Josephine Rweyemamu ambaye anafanya biashara ya kuuza chakula katika kisiwa cha wavuvi cha Mchangani anasema kuwapo kwa mamba wala watu katika visiwa hivyo kunawatisha.
Anasema kuwa kutokana na hofu hiyo ndio maana hununua maji kutoka kwa vijana wanaochota maji ziwani ambayo yapo mita 20 kutoka sehemu ambayo anafanyia biashara.
Kwa hakika, wavuvi na wafanyabiashara wa samaki bado wanafanyia katika mazingira magumu na yasiyokuwa salama shughuli zao hali ambayo inaonyesha wazi kuwa kama juhudi hazitafanyika kuboresha mazingira basi kuna uwezekano wa sekta hii kuanguka.
Ingawa sera ya uvuvi inaeleza wazi kuwa serikali itaweka mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli za uvuvi nchini na kuendeleza rasilimali zilizopo katika eneo hilo lakini hili halijafanyika.
Sekta ya uvuvi inachangia karibu asilimia 10 ya pato la taifa kwa mwaka. Ni chanzo kikuu cha protini kwa karibu theluthi moja ya watu nchini.
Ingawa serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii imekuwa ikieleza kuwa inaimarisha ulinzi wa rasilimali katika ziwa victoria , ukweli ni kwamba hakuna ulinzi wowote uliopo hususan katika eneo la ziwa lililopo mbali na nchi kavu.
Kwa mfano katika bajeti ya mwaka 2006/2007, ya wizara hiyo iliyosomwa na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Athony Diallo ilieleza kuwa doria nyingi zinafanywa Ziwa Victoria na dhidi ya uvuvi haramu
Lakini ukweli ubaki kuwa uvuvi wa kutumia zana haramu yakiwemo makokoro na nyavu zenye matundu madogo zinaendelea kutumika kama kawaida kwenye visiwa hivi.
Wavuvi wanaotumia makokoro wameamua kuhamishia shughuli zao katika visiwa mbali na nchi kavu kutokana na idara ya uvuvi kuwa haiana boti ambayo inaweza kufanya doria katika maeneo mengi ya mbali.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home