Ripoti maalum
Usafiri wa ziwa victoria ni hatari tupu
* 158 wamekufa maji mwaka huu
* Wengi wanatumia mitumbwi
*Vyombo vingi vya usafiri ni chakavu
UNAPOANZA safari ya kutumia usafiri wa boti au mitumbwi inayotumia injini kutoka Mwanza mjini kuelekea katika visiwa vinavyotumiwa na wavuvi katika ziwa Victoria hivi sasa, picha inayokujia haraka haraka katika akili yako ni ajali ya meli ya Mv Bukoba iliyotokea mwaka 1996 karibu na bandari ya Mwanza kuua watu karibu 900.
Kumbukumbu ya ajali hiyo itakujia kutokana na ukweli kwamba mbali ya kutokuwa imara boti au mitumbwi hiyo inapakia mizigo kuliko uwezo wake.
Sababu kubwa iliyosababisha ajali ya meli ya MV Bukoba kuzama ni kupakia mizigo mingi kuliko uwezo wake.
Kutokana na mitumbwi mingi ya inayokwenda katika visiwa hivyo kupakia abiria na mizigo mingi imekuwa ikisababisha vyombo hivyo vya usafiri kuzama na kuua watu wengi.
Watu wengi wanaokwenda katika visiwa hivi wanalazimika kutumia usafiri huu wa boti na mitumbwi pamoja na mizigo kutokana na kukosekana usafiri wa uhakika wa meli kubwa kuwafikisha katika visiwa hivyo ambavyo vingi vipo umbali wa kilomita zaidi ya 100 kutoka Mwanza mjini.
Usafiri wa boti kubwa ambazo zinafanya safari katika baadhi ya visiwa vikubwa nao hauna uhakika kutokana na wamiliki wa boti hizo kupanga safari kwa matakwa yao.
Mmoja wa wavuvi anayefanya shughuli zake katika kisiwa cha Mchangani kilichopo katika Wilaya ya Sengerema, Mahuma Lugeje anasema kuwa kitendo cha wamiliki wa boti kubwa kupakia mizigo mingi mno ya samaki wabichi na abiria kunaweza kuisababisha kuzama.
Anasema boti nyingi kubwa zinazofanya safari zake katika baadhi ya visiwa vikubwa zimechakaa kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu, hivyo nazo hazina uhakika.
"Safari za kufika katika visiwa hivi zinatisha kwa sababu ukweli ni kwamba hatuna uhakika wa usafiri wa kutufikisha huku, " anasema na kuongeza "kama hakutakuwa na utaratibu wa haraka wa kuletwa usafiri wakueleweka ipo siku maafa makubwa zaidi yatatokea."
Anasema boti nyingi zinapakia mizigo mingi kiasi kwamba abiria hukosa nafasi za kukaa na kulazimika kukaa juu ya mizigo hali ambayo ni hatari kwa maisha yao.
Aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Maji na Nchi kavu (SUMTRA) kuhakikisha kuwa inaboresha usafiri wa kwenda katika visiwa ili kuepuka maafa zaidi kutokea.
Mwandishi wa makala hii ambaye nilisafiri hivi karibuni kwa kutumia usafiri wa boti na mitumbwi kutembelea visiwa mbalimbali vilivyopo katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza nilishuhudia hali siyo ya kuridhisha ya usafiri wa kufikika katika baadhi ya visiwa.
Kwa mfano kutoka Kisiwa cha Mchangani kwenda Mwanza mjini, nilisafiri kwa kutumia boti kubwa ambayo iliwasili katika kisiwa hicho saa 8.00 usiku iikiwa imejaa mizigo na abiria wengine wakilazimika kukaa juu ya mizigo na kwenye upenu wa nje ya eneo la kukka abiria.
Watu walikuwa wamejaa hakuna mahali pa kuweka miguu, huku harufu mbaya ya samaki iliyochaganyika harufu ya mizigo mingine ilikuwa imetanda kila mahali kwenye boti hii.
Ilikuwa bahati tu kwamba mpaka tunafika Mwanza mjini saa 1.00 asubuhi ilikuwa hakuna mvua mbayo ilinyesha vinginevyo wengi wangefika wameloma chapachapa kutokana kukosa nafasi za kukaa katika sehemu ya ya kujikinga na mvua.
Ingawa ndani ya boti hii katika eneo la kukaa abiria kulikuwa na screen ya video ambayo ilikuwa ikionyesha picha mbalimbali, lakini wengi hawakuwa na hamu ya kuingali kutokana kubanana na wengi wakitokwa jasho ingawa waliokuwa nje walikuwa wakilia upepo mkali wa uliokuwa ukiwapiga.
"Jamani hebu angalia jinsi ambavyo tumewekwa kama magunia ya samaki kwenye boti hii, hivi kweli kama ikizama atabaki mtu, hapa?," alisema abiria mmoja ambaye alikuwa akitokwa jasho huku akiwa amebanwa mbavu na wenzake.
Hata hivyo, abiria huyo alinyamazishwa na makelele ya watu waliokuwa nje wakiwa wamepigwa upepo mkali wakimwambia kama anadhani kubwa ni shida basi aende nje akaonje upepo mkali uliokuwa ukiwapiga.
Karaha ya usafiri katika boti hii ilimfanya kila mmoja kuvaa sura ya kinyama, kila ambaye aliguswa na mwezake au kukanyagwa kwa bahati mbaya ilikuwa kama vita, matusi ambayo yalitoka huwezi kuyategemea ili mradi kila mmoja alikuwa akiugulia kivyake maumivu ya usafri huo.
Ingawa maumivu yalikuwa makubwa ndani ya boti hii, lakini kwa wasafiri waliotoka katika kisiwa cha Mchangani maimivu ya usafiri huo waliyaanza mapema asubuhi.
Watu katika kisiwa hiki waliokuwa wakitaka kusafiri kwenda mjini Mwanza walianza kujindaa kuisubiri boti hiyo kuanza saa 1.00 jioni, lakini walijikuta wakianza safari hiyo saa 9.00 usiku.
Wengi walilazimika kukesha macho wengi baa wakipata vinywaji wakati wakisubiri boti na wengine wakilazimika kurejea kwenye vyumba vyao vya nyumba za kulala wageni zilizopo katika kisiwa hicho ambazo zilizojengwa kwa kutumia mabanzi ya miti.
Inawezekana wengi waliachwa kutokana na boti hiyo kuwa na mlio mdogo wa honi ya kuashiria kuwa imefika kutokana na makel;ele mengi ya jenereta zinazozalisha umeme katika kisiwa hiki.
Hata hivyo, kitu cha chakushangaza ni kwamba wengi wa wakazi wa visiwa hivi hawana ratiba maalum ya boti hizi.
Tangu asuhubi kila mmoja katika kisiwa hiki alizungumza hadithi yake kuhusu usafiri wa boti ya kwenda Mwanza siku hiyo. Wengine walifikia mahali kueleza kuwa hapakuwapo na usafiri siku hiyo kutokana na boti hiyo ilipita siku iliyofutia.
Hata hivyo, saa 9.00 usiku ilipotia nanga katika gati ya kisiwa hiki ilionekana wazi ikiwa imejaa mizigo kiasi kwamba kila mmoja akiwaza wapi atakwenda kukaa.
Wafanyakazi wa boti hiyo walikuwa wakipakia mizigo bila ya kungalia usalama wa abiria waliokuwamo ndani. Wabeba mizigo ya magunia ya samaki wabichi hawakuangalia kama kuna abiria waliyatupa ovyo huku wakiwahi kuchukua mingine iliyokuwa bado haijaingizwa ndani.
Hapa ilikuwa hatari tupu, hapakueleweka kitu, kila mmoja alitumia nguvu zake kujipenyeza kuingia katika boti hii hukua akiagalia asije kutupiwa nguania la samaki.
Kuna mama mmoja alikuwa na begi lake la nguo aliliweka chini miguuni mwakeili apate nafasi ya kuliweka lakini kabla hajapata pa kuliweka liliangushiwa gunia la samaki na mbeba mzigo, alipohoji kuhusu kitendo hicho alizawadiwa matusi ya nguoni na kuambiwa kama hataki kusafiri ashuke.
Hii ndio hali halisi ya usafiri wa boti kubwa wa kwenda katika visiwa vikubwa za wavuvi vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Mwanza, Kagera na hata Mara.
Usafiri huu wa boti kubwa ndio unaotegemewa zaidi na wafanyabiashara kusafirisha samaki kupeleka kwenye viwanda vya samaki mjini Mwanza, hata hivyo usafiri unaotumika zaidi kufika katika visiwa vidogo vigodo ni mitumbwi inayotumia injini.
Mitumbwi hii mbali ya kuwa haina nafasi kubwa lakini imekuwa ikitumika kubeba abiria na mizingo mingi zaidi ya uwezo wake kwenda na kurudi katika kisiwa hivi.
Mmoja wa wavuvi katika kisiwa cha Zilagula, Simon Chenye anasema kuwa ajali ya mitumbwi kuzama wakati wa kusafiri ziwani ni jamba kawaida.
Anasema matukio mengi ya watu kuzama ziwani hutokea wakati wa msimu wa masika ambapo mvuya nyingi hunyesha azikiambatana na upepo.
Hata hivyo, anasema kuwa wa watu wanalazimka kutumia usafiri wa mitumbwi kwenda katika visiwa kwa sababu hawana manna nyingine ya usafiri wa kuwafikisha huko.
Tatizo la usafiri wa kufika katika visiwa hivi linaungwa mkono na Afisa mistu wa wilaya ya Sengerema ambako visiwa hivi vipo, Ernest Mkilindi ambaye anakiri kuwa tatizo hilo limekuwa likimwamisha kufika mara kwa mara katika visiwa hivyo kwa shughuli za kikazi.
Asema kimsingi visiwa vyote vilivyopo ziwa Victoria upande wa Tanzania vinavyotumiwa sasa na wavuvi kama kambi zao ni hifadhi ya mistu ya serikali.
Mkilindi anasema hivi sasa usafiri pekee wa kufika katika visiwa hivyo ni wa boti ambayo mara nyingi huwa mbovu hivyo kufika katika visiwa hivyo huwa kwa nadra sana.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi wa SUMATRA mkoa wa Mwanza, Kapteni King Chiragi zinaonyesha kuwa jumla ya watu 158 wamekufa maji na wengine 95 wamenusurika baada ya vyombo walivyokuwa wakisafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza kati ya Januari na Oktoba mwaka huu.
Chiragi anasema kuwa ajali hizo zilitokea ama kutokana na uzembe wa manahodha, wamiliki wa vyombo au uchakavu uliotokana na kutozingatia masharti ya usafiri na usafirishaji ziwani.
Hivi karibuni meli ya meli ya MV Nyamageni ilizma katika Ziwa Victoria wakati ikiwa inasafiri kati ya Mwanza na Bukoba na kuua watu zaidi 50 waliokuwamo kutokana na kupakia mizigo zaidi ya uwezo wake.
Matukio mengine ya ajali za usafiri wa ziwani yaliyotokea mwaka huu ni pamoja na boti ya mwendo kasi ya Lake Fast Ferries Ltd kuzimika ghafla katikati ya Ziwa Victoria ikiwa na abiria 50 wakati ikifanya safari zake kati ya Mwanza na BUkoba mkoani Kagera.
Hata hivyo, matatizo ya usafiri wa kuelekea katika visiwa hayapo katika wilaya ya Sengerema peke yake bali hata wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Kutokana na kuwa na matatizo hayo, mkuu wa wilaya hiyo Peter Toima ameiomba serikali kuipeleka boti kwa ajili ya kuwasafirisha viongozi wa wilayani hiyo ili waweze kufika kwenda visiwa ambavyo havifikiki kwa sasa kutokana na kukosa usafiri.
Toima alitoa ombi hilo hivi karibuni kwenye kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Mwanza (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza.
Anasema kuwa kulingana na mazingira ya wilaya ya Ukerewe, eneo kubwa la wilaya hiyo limezungukwa na maji lakini wilaya haina chombo cha uhakika cha kusafiria kutoka kisiwa kimoja hadi kingine hali ambayo inawafanya watendaji wa serikali kushindwa kuwafikia baadhi ya wananchi.
Naye Mbunge wa Ukerewe, Getrude Mongella anasema kuwa aliwahi kuongelea kuzungumzia suala la wabunge wa ukerewe kukopeshwa gari na boti bungeni,wabunge wakaangua kicheko lakini suala la boti kwao ni muhimu sana ingawa waliona kama ni mzaha.
Anasema kuwa kuna visiwa ambavyo viongozi wa serikali hawajawahi kufika ndiyo maana ilifikia wakati wananchi wakawa na serikali yao kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu za kisekali.
Mongella anapendekeza kuwa ili kumaliza tatizo hilo la usafiri wa kuvifikia visiwa vyote vilivyopo katika wilaya yake ni vyema wapeleke kilio chao kwa waziri mkuu Edward Lowassa yeye mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. James Msekela ambaye alikubalibaliana pendekezo hilo la Mongella katika kikao cha RCC.
Ni wazi kuwa endapo mikakati madhubuti haitafanyika kuboresha usafiri wa ziwa victoria hususan wa kwenda katika visiwa vinavyotumiwa na wavuvi wa samaki basi watu wengi watakufa maji.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home