Karume acheni hizo pokeeni msaada wa Raza
Na Julius Samwel Magodi
WIKI hii kama kuna jambo la ajabu ambalo limetokea nchini ni la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kumkatalia mfanyabishara maarufu visiwani hapa, Mohammed Raza, kukarabati wodi ya watoto ya Hospitali Kuu Mnazi Mmoja na kutoa msaada wa magodoro kwa watoto.
Nasema ni la ajabu kwa sababu ni wazi kuwa hakuna mtu duniani ambaye anaweza kukata msaada wakati ana matatizo makubwa.
Hiyo ni sawa na mtu ambaye yupo karibu kufa njaa kukataa chakula kwa kuongopa kuwa chakula anacho cha kutosha hivyo hahitaji tena.
Wizara hiyo ilimjibu raza baada ya kuomba kutoa msaada kuwa maeneo ambayo amejitolea kusaidia tayari yanafanyiwa kazi.
Badala yake, Raza alitakiwa kuwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya wa Hospitali hiyo, Dk Malik Abdallah Juma, ili kuangalia maeneo yanayoweza kunufaika na msaada huo.
Nukuu mojawapo ya barua ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaeleza “ Wizara inakushukuru kwa moyo wa imani kwa vile miongoni mwa yale maeneo uliyojitolea kusaidia tayari yanafanyiwa kazi, kwa hivyo nakushauri ukawasiliane na Mkurugenzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja ili kuona maeneo yanayoweza kufaidika zaidi na msaada huo,.
Majibu hayo ya wizara yametolewa wakati hospitali hiyo ikiwa katika hali mbaya, kama ilivyoonyeshwa katika taarifa ya habari ya Televisheni Zanzibar (TVZ) Agosti 7, mwaka huu magodoro yake yakiwa yamechakaa na kujaa mende.
Katika taarifa hiyo, TVZ ilionyesha baadhi ya watoto waliokuwa wamelazwa kwa magonjwa ya kuhara na kutapika, huku uchafu ukiwa umetapakaa wodini na mende wakitambaa wodini.
Kituo hicho, kiliendelea kuonyesha jinsi magodoro na mashuka katika wodi hiyo yalivyochakaa na watoto wakilala zaidi ya wawili katika godoro moja.
Raza mwenyewe amekaririwa wiki hii akisema amesikitishwa na hatua ya wizara hiyo ya kukataa msaada wake wakati amewahi kuipatia misaada mbalimbali.
Anasema majibu ya serikali ya mapinduzi Zanzibar kuhusu kutoa msaada wake yanachanganya kwa vile mara waseme wameshapata mfadhili kabla yangu wa kupaka rangi, mara wanasema eti walikuwa na makopo ya rangi muda mrefu.
Hata hivyo, ameandika barua nyingine kwa waziri wa wizara kueleza masikitiko yake kwa kukataliwa kutoa misaada.
Kwa hakika hatua hiyo ya SMZ kumkatilia Raza ambaye alikuwa Mshauri wa Rais (Michezo) wakati wa utawala wa Dk Salmin Amour, kutoa msaada inaonyesha jinsi ambavyo bado kuna ufa mkubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Nasema kuna ufa kwa sababu inaonyesha kuwa SMZ imekataa msaada huo kwa hisia kuwa mwana CCM huyo ambaye hayupo upande wao katika siasa ndani ya chama anaweza kujipatia sifa ambazo zitanufaisha kundi lake kisiasa.
Hoja ya serikali kwamba misaada ambayo Raza alitaka kutoa tayari imeshapatikana ni mbinu za kutaka kukataa msaada kwa sababu ninaamini kabisa kama SMZ ingekuwa imeshapata mtu kukarabati wodi hiyo ingekuwa imefanya hivyo tangu zamani.
Huyo mfadhili au msamaria mwema aliyejitokeza kukarabati na kupaka rangi hospitali hiyo yuko wapi kufanya kazi hiyo mpaka ikafikia hatua ya wodi ya wototo kuwa zalio la mende na watoto kulala kitanda kimoja watu wawili mpaka watatu.
Hivi kweli SMZ inataka kutuambia kuwa mtu ambaye amejitokeza kufanya kazi hiyo anasubiri nini kuanza kukarabati?
Hata kama kuna mfadhili ambaye amejitokeza kukarabati hospitali ya Mnazi Mmoja, kwani kuna ubaya gani kama msaada wa Raza ungepokelewa halafu ukapelekwa katika kukarabati hospitali au zanahati nyingine?
Pia SMZ inataka kutumbania kwamba mfadhili akijitokeza kutoa msaada unaweza kuutakaa na kumwambia anaandike barua kuomba aelekezwe mahali pa kuupeleka! Mbona hela za nchi wahisani wakitoa kwa ajili ya mradi fulani SMZ inapokea hata kama kipaumbele chake sio mradi huo?
Hivi karibuni SMZ ilipokea shehena ya vitabu kutoka Marekani, hivi wanataka kutuambia kipaumbele chake ilikuwa ni vitabu?
Kwa hakika tukio hilo limetoa picha ya mgawanyiko mkubwa ambayo upo ndani ya visiwa vya Zanzibar.
Kwa maana nyingine ni kwamba mpasuko wa kisiasa uliopo Zanzibar ambao unatafutiwa dawa hivi sasa na serikali ya muugano chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete upo kuanzia ndani ya CCM yenyewe na upo pia mgawanyiko wa upemba na uunguja.
Inavyoonekana kutokana na chuki zilizopo kati ya wazanzibari hawa sio ajabu kabisa msaada unaoweza kutolewa na mpemba ukakatiliwa unguja kwa sababu tu aliyetoa anatoka Pemba.
Rais Amani Karume anapaswa sasa kuelewa kuwa hiyo sio njia nzuri hata kidogo ya kutawala nchi na sio utawala wa kidemokrasia.
Mgawanyiko huu anaouacha kuitafuna visiwa ndio ambao utaifanya nchi hiyo baadaye ishindwe kutawalika. Ni vyema rais Karume akaondoa vikwanzo ambavyo vimekuwa vikiwagawa wazanzibari kwa misingi ya kiitikadi na matabaka.
Kukumbatia mgawanyko kunakofanywa hivi sasa na SMZ ni kuchochea vurugu ambazo zinapotokea anayetupiwa lawama ni rais wa Jamuhuri ya Muungano kumbe mambo mnayakaroga mwenyewe.
Ni vyema pia watanzania bara sasa tukaweka sawa msimamo wetu kuhusu wanzazibari kuwa waelewe kuwa kama rais Karume ataachia chokochoko zinazofanywa na wasaidizi wake kuibua chuki miongoni wananchi na wakafikia kupigana, mchawi asitafutwe bara au kunyoshewa kidole Rais Kikwete bali mjue matatizo anayapika mwenyewe.
Mchuma janga hula na wa kawao.