Mzee wa tafakari

Wednesday, August 01, 2007

Vitambi vya ukimwi

WIKI hii serikali ilianzisha kampeni maalumu ya
upimaji wa hiyari kujua kama wananchi wameambukizwa
virusi vya ukimwi iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete
ambaye yeye na mkewe, Salma walipima jijini Dar es
Salaam wakiungwa mkono na mamia ya wakazi
waliojitokeza.

Kampeni hiyo pia ina lengo kuanza kutoa dawa za
kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs) bure kwa watu
watakaobainika kuwa wameathirika.

Mara baada ya kupima, Rais Kikwete alionyesha majibu
yake dharani ikionyesha kuwa yuko safi na mkewe na
baadhi ya wanasiasa waliopima siku hiyo baadhi yao
walitangaza majibu yao huku wengine wakikaa kimya.
Wengine walikimbia kujitokeza kupima.

Kampeni hiyo ya kupima kwa hiari sasa imeanza kuchukua
sura ya kisiasa zaidi, wengi hasa viongozi wanaotoka
chama tawala wanataka kujitokeza kupima ili
kumwonyesha Rais kwamba wako pamoja naye.

Lakini inawezekana kwamba viongozi wapinzani,
wanajitokeza kupima ili kupata imani ya wananchi kuwa
wako fiti kwa ajili ya kugombea urais katika uchaguzi
ujao.

Wakati kampeni hiyo ikiendelea, baadhi ya wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati
wakichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2007/8
bungeni Dodoma wameungana na waathirika wa ukimwi
kueleza wasiwasi wao kuhusu udaganyifu uliopo katika
ARVs.

Wabunge wanasema kuwa baadhi ya dawa za ARVs
zimeelezwa kwamba zinasababisha madhara kwa watu
wanaozitumia.

Kwa kifupi ni kwamba fedha kwa ajili ya kununulia dawa
za ARVs zinadaiwa kutumiwa kwa matumizi mengine na
nyingine kuishia kunenepesha matumbo ya wakubwa wa
serikali.

Kutokana na ufisadi mkubwa uliopo katika fedha
zinazotoka kwa wahisani hususan mfuko wa kusaidia
wenye ukimwi (Global Fund), waathirika wanapewa ARVs
ambazo zimekwisha muda wa matumizi yake na nyingine
ambazo haziwapi madhara makubwa.

Baadhi ya dawa hizo zinadaiwa kusababishia athari
mbalimbali watumiaji ikiwamo kukua matiti na makalio,
kuathiri mwenendo wa kula na kuwafanya wawe na matumbo
makubwa kiasi kwamba wanawake huonekana kama
wajawazito na wakati mwingine huwaongezea hamu ya
kushiriki vitendo vya ngono.

Kwa hakika malalamiko haya ni mazito ambayo serikali
inapaswa kuyatolea maelezo ya kina ili wananchi wajue.


Si wabunge wenye hofu kuhusiana na malalamiko hayo,
bali wananchi wote wanataka kujua serikali
imeshushghulikia vipi tatizo hilo na watu wanaokula
fedha za ukimwi.

Ninasema hivyo kwa kutambua jinsi matumizi ya ARV
yalivyo tete na kwa kuzingatia kwamba mtumiaji
anapaswa azitumie kwa maisha yake yote huku
akizingatia masharti na ushauri wa madaktari kuhusu
aina ya vyakula na dawa za kutumia.

Katika mazingira kama hayo mategemeo makubwa ya
mwathirika ni katika matumizi ya ARVs sahihi. Iwapo
ARVs hizo zinaleta madhara, ni wazi kwamba serikali
inawaandalia vifo vya haraka watu hao bila wasiwasi.

Ni vyema sasa kwa Serikali kusikiliza kilio hicho na
kutoa maelekezo sahihi kabla watumiaji hawajaingiwa
woga na kuacha kuzitumia, kama baadhi yao
walivyotishia.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home