Mzee wa tafakari

Wednesday, August 08, 2007

CCM kumfia mikononi Rais Kikwete


WIKI hii Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilifanya maamuzi mazito yakiwemo kuridhia kuwatimua madiwani watano wa chama hicho, kusimamisha viongozi wote wa Jumuiya ya Wazazi, maafisa wengine wa chama kutoka ofisi ndogo Lumumba jijini Dar es Salaam na Makao Makuu Dodoma.

Pia Kamati Kuu katika kikao chake kilichofanyika kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu wiki hii, imetangaza kumvua haki ya
kuchaguliwa katika uongozi wa CCM, Thomas Nyimbo, baada ya kuthibitika kuwa tabia na mwenendo wake havifai.

Nyimbo alikuwa ni mmoja wa wagombea wa kiti cha uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa. Hivi karibuni Nyimbo amekuwa akitoa shutuma nyingi dhidi ya mgombea wenzake.

Wengine waliosimamishwa uongozi na kamati hiyo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abiuod Maregesi, Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo,Ramadhan Suleiman Nzori, Babilas Mpemba na Katibu Mkuu, Cosmas Hinju, kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za jumuiya hiyo.

Mtu mwingine aliyekutana na makali ya panga la kamati hiyo ni Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Mujuni Kataraiya ambaye ametagazwa kufukuzwa kazi kutokana tuhuma za ubadhirifu wa mali za chama wakati alipokuwa Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mwanza.

Kwa hakika maamuzi hayo ni mazito kwa chama hicho tawala kuwahi kuyatoa katika siku za hivi karibuni.

Swali tunalojiuliza hivi kweli CCM imeaamua kuzaliwa upya kutokana na kuamua kuanza kuchukua hatua za kuwashughulikia wabadhirifu wa mali zake au ni maamuzi ya kisiasa ambayo yamejifichia katika ubadhirifu?

Nasema hivyo kwa sababu kwa miaka yote CCM ndiyo ambayo ilikuwa chama ambacho kilisifika kutokana na kukumbatia ufisadi, hakuna hatua ambazo zimewahi kuchukuliwa kwa watu ambao wamehusika katika kuua miradi yake mikubwa ya uchumi.

Ilifikia mahali hata watumishi wa serikali waliokuwa wakifilisi mali za umma, badala ya kufukuzwa walipewa ulaji mwingine kwa kupewa mashirika mengine kuyaongoza. Kisa kanda wa CCM!

Leo kufumba na kufumbua tunaona CCM ile ile tuliyoizoea inaibuka na maamuzi mazito kama haya ya kuwatimua kazi wabadhirifu wa mali zake. Kwa hakika umetuachia maswali mengi ya kujiuliza.

Wapo wanaofikiria kuwa uamuzi wa kuwasimamisha viongozi wote wa jumuia ya wazazi ni wa kisiasa zaidi kutokana na juimuia hiyo viongozi wake hawakuwa kambi ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Hisia zilizopo ni kwamba walioadhibiwa katika kikao hicho ni wale tu ambao walionekana kuwa hatari katika ustawi wa mtandao wa Rais Kikwete uliomwigiza madarakani.

Ingawa kamati kuu imetangaza rasmi kuvunja mtandao ndani ya chama hicho lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wanaoendelea kumzunguka rais na kumpa ushauri ni wale wale wana mtandao ambao leo ndio wanaomshauri Rais vibaya katika uendeshaji wa uchumi na masuala mengine.

Lakini wana mtandao hao mbali ya kumzunguka rais lakini wana ajenda nyingine ya kutengeneza rais wa Tanzania wa baada ya rais Kikwete kumaliza muda wake.

Dhambi kubwa ambayo imewaponza watu hao walioadhibiwa ni kuwa na mtizamo toafuti ndani ya chama hicho. Ingawa hao wameadhibiwa lakini hiyo imetumika kama njia yakuwatisha wengine ambao wanaonekana kuwa tishjiop la mtandao huo.

Miongoni mwa watu ambao mpaka sasa wanaonekana kukigawa chama kutokana na nguvu walizonazo ambao sio wana mtandao ni pamoja na Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Profesa Mark Mwandosya, waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, na waziri wa ardhi na maendeleo ya makazi, John Magufuli.

Kwa hakika nyufa ndani ya CCM bado ni kubwa na kwamba kama hatua za kumaliza makundi ndani ya chama hicho hazitachukuliwa haraka, huenda chama hicho kikamfia mikononi Rais Kikwete kama ataendelea kulea kundi la marafiki zake la wanamtandao.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home