Mzee wa tafakari

Monday, July 17, 2006

Washeshimiwa wasomaji wangu hapa nakueleteeni moja ya mjadala ambao nilioujadili katika gazeti la Mwananchi hivi karibuni:

Mindombinu acheni kuweka mkono mchafu daraja la Kigamboni


Hivi karibuni watanzania tulipata taarifa za kusikitisha kuhusu ujenzi wa mradi mkubwa wa daraja la Kigamboni jijini Dar es salaam. Taarifa hizo zilieleza kuwa ujenzi wa daraja hilo la kigamboni umetiwa mkono mchafu na wizara ya miundombionu baada ya wizara hiyo kuamua kuitisha zabuni nyingine ya kuufanyia upembuzi mradi huo.

Nasema umetiwa mkono mchafu kwa sababu kutokana na kitendo cha wizara ya Miundombinu kuomba fedha Benki ya dunia kufanya kazi ya upembuzi wa mradi huo wakati tayari NSSF ilifanya kazi hiyo.

Ripoti ya mandeleo ya mradi huo iliyowasilishwa kwenye kamati za bunge za miundombinu na Maendeleo ya jamii na NSSF inaeleza kuwa hatua hiyo ya wizara ya miundombinu kuomba fedha nyingine za kufanya upembuzi wa mradi umewaudhi wafadhili wa mradi huo serikali ya Uholanzi.

Serikali ya Uholanzi imeudhika kwa vile kupitia kampuni yake ya Oret ambao watatoa jumla ya euro milioni 22.5 ambayo ni sawa na asilimia 50 ya gharama ya mradi mzima, tayari wameshafanya upembuzi wa mradi huo.

Mradi mzima unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh bilioni 72.

Fedha nyingine za kugharimia mradi huo zintarajiwa kupatikana kutoka Benki ya IGN ambayo itatoa euro milioni 15, sawa na asilimia 33 na NSSF watatoa euro milioni 7.5 ambayo ni sawa na asilimia 17 .

Mradi huo mkubwa wa ujenzi wa daraja la Kigamboni ukikamilika unatatoa ajira kwa watu 12, 700 na wengine 17,300 ambao watapata ajira kwa njia ambayo sio ya moja kwa moja.

Kutokana na kutumia fedha nyingi za ujenzi wake baadhi ya watumiaji itabidi walipie kulitumia daraja hilo. Watakao lazimika kuchangia ni pamoja wenye baiskeli , mkokoteni, magari ndogo, mabasi madogo na malori.

Kwa ujumla mradi huo mkubwa wa daraja la kisasa unatarajiwa kurejesha fedha zitakazotumika kwa muda wa mikaa 17.

Mkurugenzi wa NSSF, Ramadhan Dau ambaye tayari amewasilisha malalamiko ya kukwamishwa kuanza kwa ujenzi na wizara ya miundombinu kwa kamati za wabunge za meandeleo ya jamii na ile ya miundombinu.

Kwa hakika, hatua ya wizara ya miundombonu kuanza kuingiza mkono wake katika mradi huu mkubwa, sisi wakazi wa Dare s salaam, tunaona kama ni ucheleweshaji wa makusudi kumaliza kero ya wananchi hususan wanaokaa Kigamboni.

Hivi ni kitu gani ambacho kimewafanya wizara ya miundombinu kuamua kukopa hela benki ya dunia kwa ajili ya kufanya kazi ambayo tayari imeshafanyika?

Je haya sio matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi? Ninashawishika kuamini hatua ya wizara kuomba fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi wa mradi umezigatia maslahi zaidi ya watu binafsi kuliko ya taifa.

Ninahisi kuna mtu katika wizara hiyo anataka kufaidika na fedha hizo ama kupitia kampuni ambayo itapewa kufanya upembuzi mwingine au kwa njia ya nyingine, kiasi cha kuanza kupindisha maamuzi yaliyofanywa na serikali.

Waziri wa miundombnu, Basil Mramba nadhani ni wakati mwafaka watanzania atueleze sababu za msingi zilizofanya wizara yake kukwamisha kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo.

Lakini pia uamuzi wa wizara ya miundombinu ni unapingana wazi wazi na utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM), ambayo inaeleza kuwa ujenzi huo untarajiwa kuanza mwaka huu.

Daraja la Kigamboni lilikuwa moja ya kete kubwa iliyotumiwa na mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na mbunge wa Kigamboni, Ali Mwichumu katika kujipatia ushindi.

Inashangaza leo katika serikali hiyo hiyo ya CCM, wizara moja inatokea kukwamisha utekelezaji wa ahadi walizoziahidi kuondoa kero za wananchi.

Nadhani huu unaweza ukawa ni mfano wa mamabo mengi ya maendeleo yanavyokwamishwa na watu wachache kwa maslahi yao.

Nadhani kwa jambo hili, Rais Kikwete hataliacha hivi hivi ataliingilia ili wale wanaomezea mate kutafutana fedha za mradi huo awabane au hata kuwachukulia hatua kali.

Watanzania hatuwezi kupata maendeleo ya kweli kama kila mradi mkubwa unaotekelezwa na serikali kila mmoja anakodolea macho kupata chochote kitu. Ama kupitia katika zabuni au kampuni ambazo zitafanya kazi hiyo.

Hii ndiyo matokeo ya kupewa makandarasi wababaishaji kazi ya kujenga barabara , ambazo zimekuwa hazikamiliki au nyingine zikikamailika zinagharibika katika kipindi kifupi.

NSSF waachwe wandelee na ujenzi wa daraja hili ambalo mbali ya kuondoa kero kwa wananchi pia litakuwa moja ya vivutio vya utalii.

Wizara ya miundombinu hasa waziri na watendaji wake lazima wawe wazalendo , acheni ujenzi uendelee, vinginevyo hatutawaelewa mnataka nini katika daraja hilo.

mwisho

Tuesday, July 11, 2006

Wazee wa blog! Naingia katika uwanja wenu ili tubadilishane mawazo.

naamini tutajadili mambo muhimu ambayo ni yanahusu mustakbali wa taifa letu.

Julius