Mawaziri watakaoshindwa kumudu kasi mpya watimuliwe mapema
JUZI Rais Jakaya Kikwete aliteua baraza lake la kwanza la mawaziri, likiwa idadi ya mawaziri 60 kati yao 40 ni wapya na 20 ni wale waliokuwa katika baraza lililopita.
Hata hivyo, Rais Kikwete wakati akitangaza baraza hilo alisema kuwa wakati analiunda amezingatia agenda na majukumu yaliyopo mbele ya serikali hiyo.
Pia Rais Kikwete alisema sababu nyingine ambayo imefanya baraza hilo kuwa katika muundo huo ni pamoja na kunzingatia uwakilishi na umoja wa kitaifa.
Kutokana na muundo wa baraza hilo kuwa kujumuisha mawaziri wengi angalau kila mkoa umepata waziri mmoja.
Kikwete pia akavunja baadhi ya wizara na kuziunganisha pamoja na kuunda wizara mpya kadhaa. Mbali ya kuongeza wizara pia manaibu waziri katika wizara nyingine wameongezwa idadi.
Kama alivyosema yote hayo ameyafanya kwa nia ya kuuleta ufanisi na kuwatatulia matatizo wananchi kwa njia ambayo ni rahisi zaidi.
Kwa hilo tunakubaliana nalo kwa asilimia mia moja kwa sababu Watanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakikerwa na mambo mengi bila ya kupatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, pamoja na nia njema ya Rais Kikwete kuweka mfumo mpya wa baraza la mawaziri, lakini kuwa na mawaziri wengi kunaweza kuongeza matumizi ya serikali.
Hakuna ambaye anaweza kusimama kupinga kuwa matumizi ya serikali yataongezeka kutokana na kila waziri kuhitaji kupatiwa mahitaji muhimu kutokana wadhifa wao ikiwamo kuwa kuishi katika nyumba ya serikali, gari ya kifaharai maarufu 'shangingi' na matumizi mengine ya kila siku.
Matumizi ya sasa ya serikali kwa kiasi kikubwa yanakwenda kwenye shughuli za utawala, hivyo kuongeza idadi ya wizara na idadi ya mawaziri ni wazi kuwa unawafanya watanzania wajikamue zaidi mifukoni kulipa kodi ili waweze kufidia gharama za uendeshaji za mawaziri.
Si vyema kwa sasa kushauri kupunguza idadi ya mawaziri na wizara hizo kutokana ukweli kuwa rais tayari ameshawateua mawaziri hao na kuwaapisha tayari kwa kuingia kazini.Ila kinachotakiwa hatua kadhaa za kupunguza matumizi ya mawaziri hao zichukuliwe haraka.
Moja ya eneo ambalo ni wazi linaonekena kuwa linachukua matumizi makubwa katika uendeshaji wa serikali ni magari ya fahari wanayotumia mawaziri na wakuu wa idara za serikali.
Gazeti hili lilishawahi kuandika huko nyuma kuwa serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharimia magari ya kifahari ya mawaziri na watumishi wengine wa serikali.
Ni wazi kuwa kama gharama hizo zitaachwa bila ya kupunguzwa ukitilia amaanani kuwa idadi ya mawaziri 20 wameongezeka tutaendelea kubeba mzigo mzito mkubwa amabo huenda mbele ya safari itatupunguzia kasi yetu ya kuelekea katika maendeleo ikapungua.
Ni vyema sasa tuukajiuliza kwa nini tuendelee kubeba gharama hizi? Kwa nini tusizipunguze kwa kubadilisha aina ya magari wanayotumia mawaziri? Hivi mawaziri wakitumia magari ya kawaida hawatakuwa hadhi ya kuitwa mawaziri? Nadhani hilo linawezekana kabisa kwa kuwapa mawaziri na wakuu wengine wa idara za serikali magari ya kawaida.
Kuna nchi nyingi zimeliona hilo na kuamua kupunguza gharama za uendeshaji wa magari ya serikali kwa watumishi wake kuacha kutumia magari ya kifahari na kutumia ya kawaida.
Burundi ni mfano wa nchi hizo ambayo hivi sasa imeamua watumishi wake wakiwamo mawaziri kutumia magari ya kawaida.
Kama serikali itaamua kuacha kutumia magari hayo ambayo yanatumia mafuta mengi na vipuri vyake ni gari, serikali inaweza kudhibiti kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa ofisi mawaziri.
Hakuna mtu ambaye anaweza kupigana na dhamira ya Rais Kikwete ya kuweza kuwaletea maisha bora, kinachotakiwa ni kuaangalia namna ya kupunguza matumizi.
Kwa upande wao mawaziri walioteuliwa, Rais Kikwete awape mikataba ambayo itawafanya wawajibike na kuwafanya waondokewe na ndoto kuwa sasa wameingia katika neema ya kuishi maisha ya peponi ya kupata kila wanachohitaji hata kama kwa njia ya kuwabia wananchi.
Waziri atakayeshindwa kutimiza malengo yake aliyopangiwa basi aondolewe mara moja badala ya kumhamishia sehemu nyingine au kumwacha kwa muda mrefu akiboronga. Muda wa kufanya kazi kirafiki haupo tena katika karne hii.
Naugana na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mara baada ya kutanagaza baraza la mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa ataanza kukutana mawaziri mmoja mmoja akiwa na watumishi wa wizara aliyopewa kuwapa majukumu.
Nadhani hiyo ndiyo njia pekee itakayowafanya wawajibike kuwatumia wananchi kwa kuwaletea maisha bora. watanzania tunahitaji mawaziri wachapakazi sio wabababishaji ambao watatumie fedha zetu za kodi kuwalipa mishahara na malupulupu mengine bila ya kuona wanachofanya.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home