SMZ inaogopa kivuli cha helikopita ya Mbowe?
HIVI karibuni mgombea urais kwa tikiti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliwekewa vikwazo na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kufanya kampeni zake katika ardhi ya visiwa hivyo.
Mbowe akiwa na helkopita yake alilazimika kukatiza ratiba yake ya mikutano ya kampeni visiwani humo kutokana na kinachoelezwa kuzuiwa aina ya usafiri aliokuwa akiutumia kuruka katika anga ya Zanzibar.
Mbowe mwenyewe alikaririwa na baadaye na vyombo vya habari akisema alitakiwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Karume kisha kuendesha mikutano yake kwa kutembea kwa gari.
Uamuzi wa kumzuia Mbowe kufanya kampeni visiwani uliofanywa na SMZ, umekuja wakati kampeni zinaelekea ukingoni kabla ya wananchi kupiga kura Oktoba 30 mwaka huu.
Kwa hakika uamuzi huu ni wa kushangaza kwa sababu unakiuka haki ya kila mgombea kufanya kampeni mahali kokote bila ya kuwekewa mizengwe.
Unashangaza kwa sababu kama Mbowe akiwa mgombea wa urais wa Jamuhuri ya Muungano, anaruhusiwa kufanya kampeni kila kona ya nchi ikiwamo mikoa ya Zanzibar.
Mbona wagombea wengine akiwamo mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete na wagombea wengine wa vyama vingine wanaruhusiwa kufanya kampeni visiwani Zanzibar? Kwa nini zuio liwe kwa Mbowe tu?
Ni maswali ambayo SMZ inatakiwa kutujibu watanzania hivi sasa wakati tuanajinandaa kuingia katika uchaguzi .
Mpaka sasa SMZ haijatoa sababu za kiufundi za kukataliwa kwa helikopta ya Mbowe kuruka kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kufanikisha ratiba yake ya kuhutubia mikutano iliyokuwa imepangwa na chama chake Zanzibar.
Mbowe kwa kutumia helikopta hiyo ameweza kujipatia umaarufu mkubwa na kuweza kuonekana chati yake katika mbio za kuwania urais wa Tanzania ikiwa inazidi kupanda.
Vile vile, kwa kutumia helikopita hiyo ameweza kufanya mikutano mingi kwa siku katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Mbeya, Rukwa, Singida, Dar es Salaam kutaja tu kwa uchache.
Kutokana na kupanda chati kwa haraka kwa mgombea huyo, tayari ameaanza kutajwa sana na wanasiasanchini na wagombea wengine wa uarais katika hotuba zao.
Watu ambao wameanza kumrushia makombora mgombea huyo baada ya kuanza kutumia helikopta kutoka chama tawala.
Hivi karibuni hata Rais Benjam Mkapa alikaririwa akiwataka wapiga kura wasichague mgombea huyo kutokana na sera zake za ubaguzi wa majimbo. Mbali ya Rais Mkapa hata Kikwete mwenyewe wamekuwa wakimtaja mara kwa mara wakati wa kampeni zake. Hali hii ilikuwa tofuati kabisa wakati kampeni zinaanza akiwa anatumia usafiri wa magari.
Ninashawikika kuamini kuwa huenda SMZ imzuia Mbowe kufanya kampeni zake visiwani kwa kuongopa kivuli cha helikopta.
Hatuoni sababu za SMZ kumzuia Mbowe kufanya kampeni visiwani wakati ikijua kuwa wazi kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais anayetafutwa ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa sababu ya mgombea urais kuwekewa vigingi ili asitumie njia ya usafiri anayoamini ni halali na rahisi zaidi kuwafikia wapiga kura ni vigumu kujua maana yake.
Kubwa zaidi, kwa muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa ni eneo tete katika siasa za Tanzania, ni kisiwa ambacho kimesababisha machafuko ya usalama wa uhai na mali za raia, na ni kisiwa ambacho kwa hakika kimekuwa gumzo baya kuhusu mahusiano ya raia wa Tanzania kwa sababu tu ya kupandikizwa chuki na wanasiasa wasiotaka suluhu.
Kutokana na ukweli huu, tunashindwa kuielewa vema SMZ kwamba inapokataza mgombea urais kufanya kampeni zake kwa kutumia helikopta inataka kuwaambia nini wananchi?
Inataka kutuleza kuwa kosa la Mbowe ni kutumia njia ya kisasa ya usafiri kwa ajili ya kampeni zake? Je SMZ inataka wagombea warudi katika enzi ya ujima watumie punda au mikokoteni?
Tunaamini kwamba hatua ya SMZ ya kuzuia helikopta ya mgombea wa Chadema inatokana na hisia za watu wachache wanaogopa changamoto, wasiotaka kwenda na wakati.
Ninaamni SMZ ina viongozi wazuri tu ambao watatafakari upya uamuzi wao na kuamua kumruhusu mgombea huyo kunadi sera zake kwa Wazazibari angalau katika kipindi hiki kifupi kilichobakia.
Kumzuia kutazidi kuipaka matope Zanzibar katika jumuia ya kimataifa.
Alamsiki
0 Comments:
Post a Comment
<< Home