Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Kikwete kwa hilo tuko pamoja

KUNA hadithi moja ambayo imekuwa ikisimuliwa tangu enzi ya mababu ya familia mbili ambazo zilikuwa na taratibu tofauti za kuishi.

Inasimuliwa kuwa kulikuwapo familia mbili zilizokuwa zikikaa pamoja moja ilikuwa ikiongozwa na baba mkali na nyingine ya mzee mpole.

Mzee Mkali katika familia yake aliweka masharti kadhaa kuhusu wageni waliokuwa wakija nyumbani kwake kutembelea. Mojawapo ya masharti ilikuwa ni wageni kutoingia chumba chake cha kulala, mgeni kubisha hodi kabla ya kuingia ndani, kutokula chakula kabla ya kukaribishwa na mgeni kutopata taarifa muhimu za kuhusu ulinzi wa nyumba..

Wakati familia ya Mzee Mkali ilijipatia heshima kubwa kutokana na msimamo huo, Mzee Mpole hakuweka masharti yoyote kwa wageni, kwa madia kuwa kuweka masharti kwa wageni ni ubaguzi na kinyume cha utamaduni wao. Wageni waliruhusiwa kuingia katika nyumba ya familia hiyo bila kuwekewa masharti. Waliruhusiwa kuingia kuanzia sebuleni na kutokea chumba cha kulala cha Mzee Mpole. Mgeni alifanya anachotaka bila ya kuulizwa.

Waliishi hivyo kwa miaka mingi, lakini ilitokea wakati familia hizo, zikagombana na kufikia kupigana vita. Familia ya Mzee Mpole ilishindwa vita kutokana na familia ya Mzee Mkali kuwa na mbinu nzuri za kivita ambazo hazikujulikana familia ya ya Mzee Mpole. Mzee Mkali alitumia upinde kuwarushia mishale na kuwaua maadui akiwa kwa mbali wakati Mzee Mpole na familia yake walitumia silaha duni za fimbo ambayo ziliwafanya washindwe kuua maadui.

Baadaye ilikuja kubainika kuwa Mzee Mkali alishinda vita kutokana na kujua adui yake anamiliki silaha za aina gani na akajiweka sawa.

Kwa nini Mzee Mkali alijua familia ya Mzee Mpole ina aina gani ya silaha? Ni kutokana na kukosa utaratibu wa kuigiza wageni ndani ya nyumba. Wageni kutoka familia ya Mzee Mkali waliingia mpaka chumbani na kuona aina ya silaha walizokuwa wanazo.

Kwa hakika mfano huo unafanana kabisa na hali ambayo ipo hapa nchini kuhusu utaratibu wa kukaribisha wageni.

Tanzania hivi sasa ni sawa na familia ya Mzee Mpole ambayo ina waachia wageni kuingia mpaka chumbani. Wageni hivi sasa wanaingia holela kufanya biashara na kazi bila hata ya kuulizwa na mtu.

Kauli ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete kuwa akifanikiwa kuingia madarakani serikali yake itapitia upya sera ya uwekezaji ili kudhibiti wimbi la raia wengi wa kigeni kuingia holale nchini na kufanya kazi, ni mwafaka na inafaa kuungwa mkono.

Kikwete akiwa katika kampeni zake za mwisho mwisho mkoani Morogoro wiki hii alisema lengo la serikali yake ijayo halitakuwa kukataza wageni kuja kuwekeza nchini, isipokuwa hawatakiwi kufanya kazi ambazo watanzania wanaweza kuzifanya.

Alitoa mfano kuwa kuna wafanyakjazi wengi wa kigeni katika hoteli za Ngorongoro na serena za mkoani Arusha na kazi wanazozifanya zinaweza kufanywa na watanzania.

Kwa hakika Kikwete kwa suala hilo naamini utawakuwa umewagusa watanzania wote. Hakuna nchi ambayo unaweza kuingia kihuni na kupata ajira bila ya kufuata taratibu.

Kutokana na upole wetu watanzania hivi sasa nchi yetu imekuwa ni eneo huru ambalo mtu yoyote anaweza kuingia na kufanua chochote bila hata mamamala zinazohusika kuhoji.

Kuna wageni hivi sasa wanafanya kazi za kuuza nyanya, pipi maua na hata karanga mitaani kwa mwavuli kuwa ni wawekezaji. Gazeti hili lilishawahi kuandika habari pamoja na kuchapisha picha ya Mchina ambaye alikuwa akiuza karanga eneo la Feri jijini Dar es Salaam.

Hivi kweli watanzania hawana uwezo wa kuuza karanga mpaka tumtafute mtalaam kutoka nje? Hivi kweli watanzania wamekosekana wa kulinda viwanda na migodi mpaka watafutwe watu kutoka Afrika Kusini na Cananda waje kufanya kazi hiyo?

Hivi kweli wasukuma, wakwele na wabondei hawawezi kuajiriwa kufweka majani ya uwanja wa ndege wa mwekezaji mpaka aajiriwe mtu kutoka uarabuni au Australia?

Kama watanzania tulikuwa familia ya Mzee Mpole sasa tuamke na kulinda nchi yetu na kwamba taratibu za kuruhusu wageni kuingia zifuatwe. Hivi sasa kutokana na kutokuwa hata na vitambulisho vya uraia sio rahisi hata kumtambua mtu asiyekuwa raia.

Mtu yoyote ambaye atafanikiwa kuingia madarakani, anapaswa pia kuingalia vyema idara ya uhamiaji. Idara hii imekuwa kibogonyo haina meno, hata pale inapokamata wageni baadhi wamekuwa baada ya siku mbili wanaonekana wanadunda mitaani. Tunafikiri kuna kasoro kubwa katika idara hii.

Kama tutaendelea na utaratibu huu, basi siku moja nchi hii haitakuwa na mwenyewe itakuwa ni ya wageni.

Kitu kingine ambacho ninaomba kumtahadharisha raia ambaye ataingia ikulu baada ya uchaguzi kuliogopa kama ukoma hiki kitu kinachooitwa shirikisho jipya la nchi za Afrika Mashariki.

Kama nilivyowahi kusema huko nyuma kuwa kuna wenzetu wanataka kutumia shirikisho hilo kutumia rasmali zetu, kumaliza matatizo ya ajira na ardhi na baadaye kutuacha hatuna kitu. Hawa watu hawataki shirikisho wana ajenda yao kibindoni.

Watanzania bado tuna kumbuka watu hawa wanaotaka shirikisho hili leo kwa uti na uvumba ndio hao hao walilikataa na kulivunja mwaka 1977.

Wapo watu kama akina Rais Yoweri Museven wa Uganda ameshatamka wazi kuwa anataka kuondoka madarakani baada ya kuundwa kwa shirikisho la Afrika Mashariki.

Inaonekana madaraka ya urais nchini mwake ambayo anayashikiliwa kwa nguvu zote anataka kuyatumia kama ngazi ya kufikia ndoto yake ya kuwa rais wa Afrika Mashariki. Watanzania tunasema hiyo ni itabaki ndoto tu!

Rais ajaye asikubali katika kuingia katika shirikisho hilo, ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki ubaki katika kushirikiana katika ushuru wa forodha na mambo madogo madogo kuzifanya nchi zetu kuwa nchi moja.

Ninajiuliza hivi tusipoingia katika shirikisho hilo tutapoteza nini?

0 Comments:

Post a Comment

<< Home