Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Kikwete wala rushwa usiwape muda

WIKI hii Rais Jakaya Kikwete alisema anawajua kwa majina watumishi na watendaji wengine wa serikali wanaokula rushwa na kwamba alichofanya ni kuwaweka akiba ili wajisahihishe.

Alionya kwamba alikuwa hazungumzi kwa utani anajua anachosema na kwamba anapotembelea wizara na kuonya watumishi waache rushwa anawajua kwa majina.

Kikwete alisema kuawa anatoa muda kwa watu hao wajisahihishe na kwamba mwenye na asikie.

Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nelson Mandela mjini hapa, Rais Kikwete alisema mfanyakazi anayetekeleza kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi yake, serikali inaweza kumtunuku nishani, lakini haitakuwa na muda na yule atakayekwenda kinyume.

Hata hivyo, alisema serikali haina ugomvi na mtu wala chuki ila inachotaka kutoka kwake ni utumishi wake uliotukuka.

Kwa hakika ninampogeza Rais Kikwete kwa kulizungumza tatizo la rushwa kwa uwazi na hata jitihada zake za kuwajua kwa majina vigogo wa rushwa katika sehemu mbalimbali za kazi nchini.

Nasema anafaa kupongezwa kwa sababu katika vita kitu muhimu ni kumfahamu adui yako kwanza yupo wapi na anasila zipi, kwa rais Kikwete hili tayari analijua halitamsumbua kitu.

Hata hivyo, ninadhani kuwa kwa vile rais Kikwete tayari majina anayo ya watu wanaojihusisha na rushwa hana haja kuwapa muda wa kujirekebisha aanze kuwashughulikia.

Kuwapa muda ni sawa na kuwapa muda wa kubuni mbinu nyingine ya kujihusisha na rushwa kwa njia ambayo inaweza kuwa mbaya zaidi.

Labda kitu cha kujiuliza ni kuwa hawa wala rushwa wameaanza kula rushwa lini? inawezekana kabisa wengine hivi sasa ni wazee ambao wamefanya kazi hiyo kwa muda mrefu na vitisho pekee vya serikali bila ya vitendo inawezekana pia vimeshazoeleka masikio mwao.

Nasema hivyo kwa sababu mapambano ya rushwa nchini yana historia ndefu sana. Nakumbuka awamu ya Kwanza ya Marehemu Mwalimu Julius Nyerere ilipambana vya kutosha kuhakikisha kuwa wala rushwa hawapati nafasi kupitia siasa ya azimio la arusha.

Hata hivyo, wapo wajanja waliotumia njia za ndani mchana waumini wa ujamaa usiku wanaendelea kula rushwa, ingawa inawezekana katika kiwango ambacho labda hakiweze kufananishwa na Tanzania ya leo.

Awamu ya pili ya Mzee Ali Hassan Mwinyi ilipoingia madarakani ilitangaza kuwa sasa inakuja na ufagio wa chuma wa kusafisha uchafu wote wote ikiwamo rushwa.

Kwa kwa siku za mwanzo wala rushwa hawa walitulia wakapima upepo unakwendaje ili waweze kubuni njia ya kuendelea na mchezo wao, na kwa bahati mbaya watu hawa baadaye waliendelea na mchezo bila matatizo.

Aamu ya tatu, ya rais mstaafu Benjamin Mkapa ilikuja mkakati wa kupambana na rushwa, hakuna mtu ambaye hakumbuki jinsi, Tume ya Jaji Warioba ilivyoibuka na ripoti iliyokuwa ikieleza mianya ya rushwa.

Serikali ikaapa kufa na wala rushwa, lakini baadaye nguvu za kupambana na rushwa taratibu zilianza kupungua na hatimaye tulishuhudia vigogo wawili au mmoja serikalini ndio walifikishwa mahakamani tu, waliobaki ni watumishi wa chini wa serikali waliopokea rushwa ya kuku au sh 3,000.

Kwa kuzingatia hitoria hiyo, tunadhani Mheshimiwa rais Kikwete anapaswa kuwachukulia hatua moja kwa moja badala ya kutoa muda wa kujirekebisha ambao hauana kikomo.

Rais Kikwete alitakiwa atoe muda wa kujirekebisha kwa watumishi hawa ambao unakikomo. Najua rais Kikwete ni mchapakazi ambaye kama alivyosema yeye mwenyewe amedhamiria kupambana na rushwa kikweli kweli.

Nadhani kutoa muda usio na kikomo ni kuwapa mwanya hawa wala rushwa kujiweka sawa kubuni mbinu nyingine za kuendeleaza ufisadi wao kwa vile wengi kama nilivyosema wapo ndani ya serikali yake tena wengine wapo katika nafasi ya kutoa maamuzi mazito ya nchi.

Ninapotafakari kwa kina ninadhani kuwa wala rushwa hawa wakubwa wamekuwepo karibu katika awamu zote za uongozi wa nchi uliopita na wakiendelea kuwadhurumu walala hoi, kuna haja gani kuwapa muda zaidi wakati ushahidi upo na wanafahamika?

Hivi kweli mtu tunamwona anakula rushwa ya kuifanya nchini kuingia mkataba ambao hauna maslahi ambao unaingizia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi, huku tukijua kuwa alikupokea ten percent, tumwache ajirekebishe hadi lini?

0 Comments:

Post a Comment

<< Home