Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Mramba usilie, viatu vya
Magufuli vitakupwaya!

WIKI iliyopita Waziri Mkuu, Edward Lowassa alilazimika kumwita Waziri wa Miundombinu, Basil Pesembili Mramba mkoani Lindi kutoa maelezo kwa nini ujenzi wa barabara ya Lindi-Mingoyo haujakamilika kwa muda unaotakiwa.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kushangazwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo yalionyesha wazi ni dhaifu.

Kulingana na mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo, ilitakiwa ikabidhiwe serikalini na mkandarasi anayeijenga, kampuni ya AM Kharafi Oktoba 24 mwaka huu lakini hadi sasa hakuna hata sentimita moja ya barabara hiyo iliyokwisha wekwa lami.

Uamuzi huu wa kumwita Mramba kutoka Dar es Salaam kupanda ndege kumfuata waziri mkuu, ulitokana na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, Mwita Chacha kumweleza waziri mkuu kuwa, mkandarasi amevunja mkataba na kwamba hawezi kazi hiyo ya ujenzi wa barabara katika muda uliokubaliwa katika mkataba. Kutokana na hali hiyo, mkandarasi huyo alitakiwa kupigwa faini.

Mwita alisema pamoja na kuvunja mkataba huo hadi sasa, kampuni hiyo hajapigwa faini na serikali kutokana na sababu ambazo hazijui na kwamba kama ataachiwa kujenga barabara hiyo itachukua muda wa miezi 18 kuimaliza.

Hata hivyo, kampuni hiyo ya mkandarasi kutoka uarabuni inadaiwa kuwa ina matatizo na uongozi hali ambayo imechangia kushindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Hata hivyo, Waziri Mramba baada ya kuwasiliana mkoani Lindi akijieleza mbele wa waziri mkuu alilalamika kuwa, mkandarasi huyo amekuwa jeuri haambiliki na kwamba amekuwa akifanya kazi zake bila ya kufuata taratibu.

Alisema mbali ya wizara kumtaka akamilishe kazi zake haraka lakini amekuwa akikaidi agizo hilo na kwamba hata aina ya kokoto anazotaka kuzitumia katika ujenzi wa barabara hiyo haizifai.

Kwa hakika, kauli ya Mramba kuhusu mkandarasi huyo inatuchaganya sisi wananchi. Nasema inatuchaganya kwa sababu kama waziri aliyepewa dhamana ya kusimamia shughuli za barabara, analia kwa waziri mkuu sisi wananchi tufanye nini.

Tulitegemea kuwa Mramba angetueleza kwa nini wizara imeshindwa kumchukulia hatua ikiwamo kumsimamisha na kumtafuta mkandarasi mwingine.

Najua shughuli za kusimamia barabara ni ngumu kutokana na kuwa na fungu kubwa la hela ambalo linategwa kwa ajili ya ujenzi ambalo baadhi ya makandarasi wamekuwa wakilitumia kwa kushirikiana na wafanyakazi wa wizara kulitafuna.

Mramba anapaswa sasa kufahamu kuwa kwa kupewa wizara inayoshughulikia ujenzi na mawasiliano anatakiwa kukaza msuli kuhakikisha kuwa viatu vya waziri aliyepita katika wizara hiyo, John Pombe Magufuli katika kusimamia barabara vinamfiti, vinginevyo vitampwaya muda sio mrefu.

Kama mkandarasi anavunja mkataba, Mramba anapaswa kutupatia mkandarasi mwingine mwenye uwezo ili barabara zetu ziweze kukamilika kwa wakati. Kwa mwendo huu wa serikali kushindwa kuwachukulia hatua wakandarasi wanaovunja mikataba, ujenzi wa barabara unaoendelea nchini hivi sasa hautakamilika.

Ndoto iliyokuwapo mwaka 2003 kwa kiwango cha kupigiwa chapuo na rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwa ifikapo mwaka huu kuwa mtu atasafiri kwa teksi kutoka Mwanza hadi Mtwara imeshindwa kutimia.

Kuna wakati niliandika katika safu hii kuwa ndoto hiyo haiwezi kutimia kutokana na kasi ya ujenzi iliyokuwa ikionekana kwa wakandarasi mbalimbali wanaojenga barabara zinazounganisha barabara hiyo. Lakini waziri Mramba alisema nilikuwa napigana serikali, nadhani sasa anaweza kukubaliana na mimi.

Wakandarasi wengi wanaojenga barabara zinazounganisha mtandao wa barabara hii bado hawafanyi kazi zao kwa ufanisi. Kwa mfano hivi majuzi tulisikia kuwa kampuni ya SIETCO kutoka China inayojenga barabara ya Igunga-Singida imeshindwa kukamilisha kazi yake kutokana na wabia katika kampuni hiyo kufilisika.

Meneja wa Mkoa wa Singida wa TANROADS, Paul Lyakurwa, alimwambia Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza kusuasua Januari mwaka huu na baadaye ukasimama kabisa mwezi uliopita.

Mkandarasi huyo, amesimamisha kabisa shughuli zote za ujenzi wa barabara hiyo baada ya kujenga kilomita 18 tu za lami, kati ya kilomita 113.5 anazotakiwa kujenga.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya China imeamua kutafuta wabia wengine ambao watakuja nchini kujenga. Kwa mifano hiyo inaonyesha wazi kuwa uteuzi wa makandarasi wa kujenga barabara bado sio mzuri huenda hauna chujio bora la kupata walio bora.

Kama utaratibu wetu ni mzuri ambao unaweza kutupatia wakandarasi walio bora basi, huenda utakuwa umegubikwa na rushwa kwa sababu barabara nyingi hapa nchini zimekuwa zikijengwa zaidi ya muda ambao mkandarasi amepewa na serikali.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home