Hivi sisi ni vipofu katika uigiaji wa mikataba ya kuuza mali zetu?
WIKI hii watanzania walipata faraja baada ya kusikia kwamba serikali imelirejesha Shirika la Ndege Tanzania (ATC) mikononi mwake baada ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kukubali kuiuzia hisa ilizokuwa ikizimiliki kwa bei ya dola moja ya Marekani.
Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Ali Mufuruki alisema kuwa SAA imekubali kurejesha hisa zake asilimia 49 ilizozinunua mwaka 2002 baada ya mazungumzo ya ujumbe wa Tanzania na serikali ya Afrika Kusini yaliyofanyika Agosti 29 Agosti mwaka huu.
Alisema sababu kubwa iliyofanya serikali kulirejesha shirika hilo katika umiliki wake ni kupishana kwa mipango ya kibaishara baina ya wabia wa kampuni.
Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema baada kurudishwa katika umiliki wa serikali, ATCL imebuni mkakati wa kununua ndege nne zaidi ili kulifanya shirika hilo kufikisha ndege sita hadi katikati ya mwaka ujao.
Akizungumzia hali ya kifedha ya shirika hilo, alisema linapata hasara ya Sh1 bilioni kwa mwezi hali inayoifanya serikali iendelee kulipa ruzuku ya uendeshaji.
ATCL ambayo inabakia katika mwenendo wa ubinafishaji chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) baada ya ndoa yake na SAA kuvunjika rasmi Agosti 29, mwaka huu, inatakiwa kujiimarisha kifedha ndani ya miaka miwili ili liweze kupata mbia mwingine kwa bei ya kuridhisha.
Kwa hakika kuvunjika kwa mkabata huu wa ATCL na SAA ni fundisho tosha kwamba mikataba mingi ambayo tumeingia katika kuyauza mshirika yetu haikuwa na maslahi kwa taifa bali ilikuwa ni kwa ajili ya watu wachache tu.
Nasema hivyo kwa sababu tumeshuhudia mikataba mingi ya uuzaji wa masharika yetu ambayo sasa imegeuka kuwa shubiri kutokana na watanzania wezetu ambao tumewapa dhamana ya kuuza mashirika yetu ama kuangalia zaidi maslahi yao binafsi.
Nakumbuka ATC ilipouzwa kwa SAA kila mtu alishangilia sana kwamba sasa shirika letu la ndege ambalo lilikuwa linachechemea sasa litakuwa shirika kubwa la ndege katika Afrika lenye ndege za kileo na wafanyakazi ambao wana viwango vya kimataifa.
SAA katika moja ya ahadi zake iliteua mji wa Dar es Salaam kama kitovu chake cha biashara katika nchi za Afrika Mashariki kama njia ya kuwa baadaye kiungo muhimu cha biashara kati yake na nchi za mashariki na magharibi za Afrika.
Shangwe hizo za watanzania hazikuendelea kwa muda mrefu baada ya ATCL kuanza kukumbwa na wingu la mvutano kati ya Tanzania na SAA baada ya kushindwa kutekelezwa kwa ahadi kadhaa zilizotolewa na mwekezaji.
Mlalamiko ya kwanza ya Tanzania yalikuwa kutokutekelezwa kwa makubaliano ya awali kati yake na SAA, likiwemo suala la kushindwa kuimarisha ATCL kwa kuongeza njia zake katika sehemu mbalimbali duniani kama ilivyokuwa imekubaliwa.
Mengine yalikuwa ni kwamba, SAA ilikuwa inakodisha ndege zake kwa ATCL kwa gharama kubwa kuliko bei halisi na kwamba mifumo ya tiketi, malipo na namba za ndege ilikuwa inawategemea SAA.
Kutokana na malalamiko hayo, Tanzania iliamini kuwa Afrika Kusini wanakusudia kuiua ATCL ili kupunguza ushindaji katika biashara ya usafirishaji kwa njia ya anga.
Mbali ya kushindwa kutimiza ahadi za SAA ilikuwa ikikaidi ushauri wa serikali ya Tanzania katika mambo kadhaa ambayo ilitaka yatekelezwe kwa mujibu wa mkataba.
Kutokana na mbia huyo kukaidi ushauri na kulalamika mara kwa mara kuwa amekuwa akipata hasara ili kuhakikisha shirika hilo linaendelea kuwepo hadi litakaporejea mikononi mwake, tangu mwishoni mwa mwaka jana ilianza kutoa Sh500 milioni kila mwezi.
Kimsingi, Sipingi mkakati wa serikali wa kujenga uchumi wa soko. Na pia ninaamini kuwa si kazi ya serikali kutengeneza na kuuza vibiriti na vijiti vya kuchokonolea meno lazima kazi nyingine zitafanywa na watu binafsi.
Nikirejea katika hoja yangu ni wazi kwamba ubinafsishaji wa mshirika yetu hakuna mtu anayeupinga,ila kinachopingwa hapa ni namna zoezi hilo linavyoendeshwa.
Mashirika ya umma yameuzwa kwa bei ya kutupa na kwamba hata mikataba yenyewe imekuwa kama vile ni bangi au dawa za kulevya ambayo haitakiwi kuonwa na mtu au umma kuelewa kinachoendelea.
Usiri huu ndio ambao umetufikisha katika hali hii ya mashirika yetu yakiwa katika hali nzuri lakini yanapouzwa au kukodishwa tunarejeshewa yakiwa katika hali mbaya.
Hali hiyo inatoa sura kwamba huenda rushwa katika zoezi hilo imeghubika ndio maana wapo watu ambao ni watanzania wenzetu wanatoa mashirika haya kwa watu kwa bei ya njugu huku wakielewa kuwa ni kuwafikisha watanzania katika hali mbaya.
Tunashukuru hatua ya serikali kuipitia upya mikataba ya madini ambayo imesaidia walau sasa watanzania tutapata hela kisia ingawa ukweli unabaki pale pale kuwa pamoja na kuwa madini mengi tunachopata hakiligani kabisa na utajiri huu.
Ni vyema sasa serikali ya awamu ya nne, ikajipanga upya hasa katika mikataba ya uuzaji wa mashirika au uwekezaji ili watanzania wafaidike na maliasili zao au makampuni yetu.
Pia mikataba ya uwekezaji au ununuzi wa mashirika ipitishwe na chombo kingine badala ya utaratibu wa sasa wa kupitishwa na baraza la mawaziri ambalo mwenyekiti wake anakuwa ni rais.
Kama mkataba utakuwa mbovu hauna maslahi ya watanzania ni vigumu kwa rais kuwajibishwa watalaam waliohusika katika kushauri kwa sababu hata yeye aliupitisha katika ngazi ya baraza la mawaziri.
Viongozi wa serikali wanaohusika na uuingiaji wa mikataba, sasa lazima wabadilike, wawatumikie watanzania kwa kuingia mikataba ambayo ina maslahi ya nchi. Kama watu hawa watabadilika basi yaliyotokea kwa ATC, na DAWASA yataendelea kutokea.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home