Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Polisi sasa mnaelekea kubaya!

RIPOTI ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuhusu unyama unaofanywa na Polisi dhidi ya raia, umekiweka wazi kilio cha muda mrefu cha wananchi.

Ripoti hiyo ambayo iliyotolewa wiki hii na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Robert Kisanga kwa waandishi wa habari inaeleza kwa undani jinsi polisi wanavyoshirikiana na majambazi kuwapora raia mali zao.

Jaji Kisanga katika ripoti hiyo ameeleza kuwa polisi wamekuwa wakitoa taarifa muhimu kwa majambazi zinazoyawezesha kuvamia raia na kupora.

Vile vile, alisema vituo vya polisi vimegeuzwa kuwa jehanamu kwa watuhumiwa kupigwa, kunyanyaswa na hata kulazimishwa kukiri makosa kutokana na kipigo wanachopata kutoka kwa polisi.

Kingine ambacho Kisanga alisema Tume yake imegundua ni kuwa vituo vingi vya polisi havina mahabusu na kwamba watuhumiwa wanawake wamekuwa wakilala kaunta pamoja na askari hali ambayo inasababisha kubakwa.

Tume hiyo imegundua pia kuwa hata katika vituo vichache ambavyo vina vyumba vya mahabusu, watuhumiwa watoto wamekuwa wakichaganywa na wakubwa hali ambayo inawafanya wapate manyanyaso na pengine kufanyiwa mambo mabaya na watuhumiwa wakubwa.

Kwa ujumla ripoti hii ya kwanza kufanywa na Tume hiyo, imesaidia kuanika hadharani maovu ambayo yanafanywa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi dhihi ya raia.

Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakilinyoshea kidole Jeshi la Polisi kuwa baadhi ya askari wake, wamegeuka kuwa majambazi na kwamba hata baadhi ya vituo vya polisi vimegeuzwa kuwa ni vituo vya biashara ambako haki yako lazima uinunue.

Kilichogunduliwa na Tume ya Jaji Kisanga kuwa askari wanashirikiana na majambazi ni kweli kwa sababu hakuna mtu asiyefahamu kuwa majambazi yote nchini yanafanya uhalifu kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya askari polisi.

Ukitaka kujua kuwa baadhi ya askari wanashirikiana na vikundi vya ujambazi ni majambazi yanapovamia mahali hata kama wapaita tukio linatendeka hurudi baada ya saa au mbili wakati ambapo wahalifu huwa wameshaondoka.

Hakuna asiyejua jinsi majambazi yanayoazimwa  silaha na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kwenda kufayia uhalifu kwa makubaliano ya malipo.

Kutokana na kuwepo ushirikiano mkubwa wa askari na majambazi imefikia mahali jambazi hivi sasa linaweza kukupa taarifa kuwa usiku wanakuja na wenzake kuchukua gari yako, ukitoa taarifa polisi huwa hakuna juhudi zozote zinazochukuliwa kukulinda

Jambazi hivi sasa likikamatwa likifikishwa polisi  baada ya siku mbili utaliona mitaani likiendelea kufanya uhalifu.
Kwa kweli hali ni mbaya askari polisi ambao jukumu lao ni kulinda raia na mali zao , hivi sasa wamebadilika kuwa askari ambao wapo kwa ajili ya kupora mali za wananchi na maisha yao.

Nani asiyeelewa kuwa hivi sasa ukiwa na mtuhumiwa wako unataka akamatwe ukienda polisi kutoa taarifa lazima utoe hela kwa ajili ya mafuta ya gari la doria usiku.

Haya ni mambo ya ajabu sana, wakati serikali ya Rais Benjamin Mkapa ikijitiahidi kuimarisha utalawa wa sheria, baadhi ya askari katika Jesi la Polisi wamekuwa kikwazo kikubwa cha juhudi hizo.

Kuhusu watuhumiwa wanawake, baadhi ya vituo vya polisi hivi sasa vimegeuka kuwa kichaka cha ubakaji  

Kutokana na vituo vingi vya polisi kukosa vyumba vya mahabusu, watuhumiwa wanawake wamekuwa wakiwekwa kaunta wanapokaa polisi na hivyo wengi kujikuta wakibakwa usiku na baadhi ya askari hao.

Wanawake wanaobakwa wakiwa polisi hushindwa kupeleka malalamiko yao kutokana na kupigwa mkawara mzito na pengine kubambikiwa kesi nyingine za bangi au dawa za kulevya wanapoonekana kutaka kudai haki zao.

Wananchi hivi sasa hawana imani tena Jeshi la Polisi kutokana na vitendo vya baadhi ya askari, hivyo wanapomkamata mhalifu wengi wanafikia uamuzi wa kujichukulia sheria mikononi kwa kuamini kuwa wakimpeleka polisi lazima ataachiwa.
Ili jeshi hilo liweze kurejesha heshima yake kwa raia, linapasa kuwaondoa askari wote wanaofanyakazi kinyume cha sheria zinazoliongoza jeshi hilo.

Bila kufanya operesheni ya kilisafisha , juhudi za serikali kutaka kuimarisha utawala bora na kuondoa rushwa hazitaweza kufanikiwa.
Askari polisi wanapaswa kubaki kuwa walinzi wa raia na mali zao na sio kuwa waporaji wa mali na maisha ya raia.

 

 

0 Comments:

Post a Comment

<< Home