Mwema sasa safisha polisi
RAIS Jakaya Kikwete wiki hii alifanya mabadiliko katika jeshi la polisi kwa kumteua, Said Mwema kuwa Inspekta Jenerali mpya wa polisi kuchukua nafasi ya Omar Mahita ambaye utumishi wake unakoma mwishoni mwa wiki hii.
Pia Rais Kikwete alimteua Robert Manumba kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kushika nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Rajabu Adad ambaye ameelezwa kuwa atapangiwa kazi nyingine.
Mabalidiko mengine ambayo rais Kikwete aliyafanya katika jeshi la polisi ni pamoja na kumpandisha cheo kuwa Kamishna wa Polisi na kumteua Clowding Mathew Mtweve kuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Jeshi la Polisi, akijaza nafasi inayoachwa wazi na Kamishna Wilson Mwansasu ambaye anastaafu kwa mujibu wa sheria.
Mwingine aliyeteuliwa kuiongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni ni Paul Amani Moses Chagonja, aliyepandishwa cheo kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi hadi kuwa Kamishna wa Polisi.
Rais Kikwete pia alifanya mabadiliko ya hadi ya utawala wa kipolisi katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao sasa utakuwa ukijulikana kama Kanda Maalum ya Dar es Salaam, huku wilaya zake tatu zikipewa hadhi ya mikoa.
Alimpandisha cheo kuwa Kamishna, Alfred Tibaigana na kumteua kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, akiwasimamia makamanda watatu wa polisi wa Temeke, Ilala na Kinondoni.
Kwa hakika mabadiliko katika jeshi la polisi yaliyofanywa na rais Kikwete yanakuja wakati watanzania walikuwa wakiyasubiri kwa hamu kubwa kutokana na kuongezeka kwa uhalifu ambao umekuwa ukihusishwa na askari wenyewe.
Ninampongeza Rais Kikwete kwa kufanya mabadiliko katika jeshi hilo na ninaamini kuwa mabadiliko hayo yasiishie hapo tu katika kulisafisha jeshi la polisi bali yaende kila mahali.
Sina mashaka na utendaji wa kazi wa Mwema, ambaye amekulia ndani ya jeshi la polisi hapa nchini kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Shirikisho la Polisi Duniani (Interpol) jijini Nairobi.
Ninaamini kuwa Mwema atatumia uzoefu alioupata katika kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya jeshi la polisi pamoja na interpol kuhakikisha kuwa anamaliza uhalifu nchini.
Hata hivyo, kitu kikubwa ambacho anatakiwa kukifanya kwanza ni kulisafisha jeshi hilo kuanzia ngazi za chini hadi ya juu.
Sio siri kuwa bado kuna maafisa wa juu ndani ya jeshi hilo ambao ni wachafu wanaonuka rushwa, wanaonuka halufu ya dawa za kulevya na bangi.
Ingawa yeye ni wenzake waliochaguliwa na rias kushika nyadhifa hizo ni wasafi lakini kama ataewndelea kukaa na maafisa wachafu nao watamchafua na hatimaye kurudi kule kule tulikokuwa.
Ili aweze kuweka mambo sawa anapaswa sasa kupangua safu ya makamanda wa polisi wa mikoa ambao wengi wao waaminika kuwa ndio kiini cha kuongezeka kwa uhalifu katika maeneo yao.
Baadhi ya makamanda hao tayari majina yao yameshafikishwa kwa rais yakiwa yameambatana na tuhuma zao kuhusu kujihusisha na uhalifu au kuwasaidai wahalifu kufanya shughuli zao.
Mwema tuaamini kuwa wewe ni mtanzania ambaye umekaa na jeshi hili kwa muda mrefu unajua udhaifu uliopo hivyo haitakuchukua muda mrefu kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya jeshi la polisi ili liweze kufanya kazi zake ya kulinda raia na mali zao.
Hivi sasa wananchi wamepoteza imani na jeshi la polisi kutokana na baadhi ya askari kujiingiza katika uhalifu na wengine kuwabambikia makosa wananchi ili waweze kujipatia.
Wapo askari wamefikia mahali pa kugeuka kuwa vibaka ambao wanapokutana na raia usiku mitaani wakiwa katika doria badala ya kuwapa ulinzi wanawapora vitu walivyonavyo.
Hatua hii imelipaka matope jeshi la polisi kiasi cha kuliacha uchi. Tunadhani kuwa sasa umefika wakati ambao Jeshi la polisi likiwa chini ya Mwema liwe safi ili wananchi wanaweze kurudisha imani.
0 Comments:
Post a Comment
<< Home