Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Kwa mwenendo huu, heshima yetu itarudi

SERIKALI imeanza kukagua majengo ya maghorofa yaliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchi nzima, kwa kuanzia, tunaambiwa kuwa majengo zaidi ya 500 yatakaguliwa katika wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Ukaguzi huu wa majengo unafanywa na timu maalum iliyoundwa kwa agizo la Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Timu hiyo inaundwa na maafisa wa serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ile ya Miundombinu na itafanya ukaguzi huo katika kata zote za Manispaa ya Ilala zenye majengo ya maghorofa.

Siyo siri kwamba wilaya ya Ilala ndiyo inayoongoza kwa kuwa na majengo mengi na marefu zaidi ya ghorofa kwa nchi nzima. Eneo lote la Kariakoo na katikati ya jiji, ambalo ndilo eneo nyeti kibiashara lipo chini ya mamlaka ya manispaa hiyo.

Kuundwa kwa kamati hiyo, kunatokana na agizo la Lowassa, siku chache baada ya jengo la ghorofa la hoteli ya Chang'ombe Village Inn lililokuwa likijengwa, kuporomoka Machi 17, 2006 na kusababisha kifo cha mtu mmoja. Huenda wapo pia waliojeruhiwa au kupotea!

Jengo hilo liliundiwa tume na juzi ilikabidhi ripoti yake kwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba, ikibainisha kwamba ujenzi mzima haukuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazokubalika.

Kosa jingine, ripoti hiyo imebaini ni la kiufundi ambalo ni pamoja na jengo hilo kukosa ramani ambayo ilipaswa kuthibitishwa na mamlaka husika au bodi ya ukadiriaji na usanifu majengo na kwamba hata kiwanja lilipojengwa hakikupimwa.

Kwa hakika, uamuzi huu wa kukagua majengo yote ya maghorofa ni muafaka ili kuyabaini ambayo hayakujengwa kwa kufuata taratibu.

Tukio la jengo la Chang'ombe Village Inn ` kuporomoka na kusababisha maafa limetuachia funzo kwamba huenda majengo kama hayo yapo mengi hapa nchini.

Wapo baadhi ya watu hapa nchini kutokana na uroho wa kupata fedha wamekuwa wakijenga majengo ya ghorofa bila ya kufuata taratibu ikiwamo kutokuwa na kibali halali cha ujenzi, kutumia wakandarasi feki.

Baadhi yao, tunasikia kwamba wanatumia hata vifaa duni ambavyo haviendani na taratibu za ujenzi wa nyumba, hususan maghorofa.

Kwa ujumla, nyumba zilizojengwa kwa mtindo huo ambazo naamini nyingi hapa nchini ni bomu ambalo likilipuka litaleta madhara makubwa kwa wananchi.

Lakini, ni nini kilichotufikisha hapa? Rushwa ni sababu kubwa kuliko sababu yoyote. Baadhi ya maafisa wa ardhi wengi kwa muda mrefu wamekuwa wakigawa viwanja kwa ajili ya ujenzi mijini kama njugu bila ya kuangalia ramani za mijini na taratibu nyingine zinazoongoza ujenzi.

Watu hawa wamekuwa wakijipatia fedha nyingi za hongo kutoka kwa matajiri hao wanaopindisha sheria ambao ndio wameingiza nchi katika migogoro mikubwa ya ardhi inayoendelea kufukuta nchini.

Hivyo, naamini kuwa hatua hii ya sasa ya serikali kuanza kukagua majengo itafichua mengi na ndiyo njia pekee ya kunusuru maisha ya Watanzania wengi ambao baadaye wangeangukiwa na majengo hayo.

Ni kutokana na ugawaji mbaya wa viwanja unaofanywa na baadhi ya maafisa wa ardhi ndio ambao umeifanya serikali katika Manispaa ya Kinondoni kuchukua uamuzi wa 'kubomoa' majengo mawili ya ghorofa nane kila mmoja yaliyopo eneo la bahari ya Hindi la Masaki jijini Dar es Salaam. Majengo hayo yanadaiwa kujengwa bila ya kufuata taratibu.

Watanzania, lazima tukubali hatuwezi kupata maendeleo kama kila mmoja ataamua kujifanyia jambo lake bila ya kufuata taratibu. Huwezi kuamua leo ukajenga nyumba mahali kokote hata kama haparuhusiwi kwa sababu tu una hela!

Kama hali hii itaachiwa iendelee sio ajabu siku moja tukiamka asubuhi na kukuta katikati ya barabara ya Mandela au Morogoro linajengwa ghorofa ambalo ni mali ya mwekezaji.

Hatua hii ya serikali ya awamu ya nne kuamua kuanza kukagua ujenzi wa majengo naamini utasaidia kuyaondoa majengo ambayo yamejengwa kinyume cha sheria na kuiweka miji yetu katika hali inayotakiwa.

Vile vile, hatua hii ya serikali itawaondolea kiburi matajiri ambao wanatumia fedha zao kupindisha sheria na kujifanyia mambo wanavyotaka. Kwa hakika, heshima itarejea kila mtu ataheshimu mamlaka zinazohusika.

Miji yote mikubwa duniani inaonekana mizuri ikiwa katika mpangilio ikipambwa na majengo marefu ya ghorofa, lakini haikujengwa holela kama ilivyo hapa kwetu, ramani ya mipango miji ilifuatwa pamoja na taratibu nyingine za ujenzi.

Wapo baadhi ya watu hivi sasa hapa kwetu bila ya kujali ramani ya mji wanajenga juu ya mabomba maji ya kunywa, maji machafu na kadhalika na wengine wanavamia viwanja vya wazi na wengine wanajenga hata chini ya nyaya za umeme wenye msongo mkubwa kana kwamba hawajui athari zake. Naamini, sasa watakuwa wameanza kupata somo.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home