Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Museven toto tundu linaloota usultani

MACHO na masikio ya watanzania kwa karibu siku 20 yalikuwa katika visiwa vya Zanzibar ambako uchaguzi mkuu wa rais na madiwani ulifanyika.

Uchaguzi huo ambao ulimazika Oktoba 30, 2005 kwa Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Aman Karume kuibuka mshindi baada ya kumshinda mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulikumbwa na misukosuko kadhaa ikiwamo CUF kukataa matokeo kwa madai kuwa hakufanyika katika mazingira yaliyohuru na haki na baadhi ya nchi za magharibi kama Marekani na Norway kuelezea kuwa hakuwa huru na haki.

Wakati watanzania tunatathimini hali ya tete za kisiasa Zanzibar, habari nyingine za kushangaza tulizipata kutoka kwa ndugu zetu waganda kuwa Rais Yoweri Museven amechaguliwa na chama chake cha NRM kuwa mgombea urais.

Habari hizo zinashangaza kwa sababu, Museven ameanza harakati za kupata nafasi hiyo kwa muda mrefu, ingawa amekuwa akitaka umma uelewe kuwa wanganda ndio wanaomtaka aendelee kuwaongoza.

Harakati za Museven kuwania nafasi hiyo, zilianza baada ya kuibadili katiba ya nchi hiyo ili kumruhusu aweze kuwania nafasi ya urais kwa kipindi cha tatu.

Uamuzi huo wa Museven ulipigiwa kelele sana na baadhi ya waganda wapenda demokrasia na jumuia ya kimataifa, lakini aliziba masikio yake na nta na kupuuza yote aliyoshauriwa.

Baada ya watu kupiga kelele na kuonekana kuwa Museven ameziba masikio yake, waliamua kutulia na kumwachia aendelee na safari yake ya kuelekea kwenye udikteta.

Tukio la hivi karibuni la Mwanasiasa maarufu nchini humo, Dk. Kizza Besigye kurejea Uganda limezidi kummwonyesha Museven sura yake halisi tofauti na tunayemjua kijana wa Mwalimu Julius Nyerere ambaye amedumu katika utawala wa nchi kwa takribani miaka 20.

Serikali ya Museven wiki hii iliagiza kukamatwa kwa mpinzani wake wa kisiasa Dk. Besigye kwa madai ya kutaka kupindua serikali akishirikiana na wenzake 14 na kumbaka msichana na kumwambukiza ugonjwa wa ukimwi.

Kitendo hicho kimelaaniwa na waganda na jumuia ya kimataifa kwani ni dhahiri kuwa kesi hiyo dhidi ya Dk. Besigye ya kisiasa zaidi kutokana na nia yake ya kutaka kugombea urais kupitia kambi ya upinzani.

Tayari Dk. Besigye ambaye hapo awali alikuwa swahiba mkubwa wa Museven amefikishwa mahakamani kujibu mashataka ya kubaka na uhaini.

Kwa hakika kama nilivyowahi kumzungumzia Museven katika safu hii, ameonyesha dhahiri kuwa demokarsia kwake ni ndoto ya mchana.

Kudhihirisha kuwa Museven ni mtu ambaye hataki demokarsia na anataka kuufanya urais wa uganda kuwa ni usultani katika muda wote aliokaa madarakani, ameshindwa katika utawala wake hata kuruhusu kuwapo kwa vyama vingi zaidi ya kuruhusu vikundi vya vugungungu la kisiasa.

Mipango ya Museven anayoendelea nayo kuwaziba midomo wapinzania wake inatisha na kwamba watanzania sasa umefika wakati kumtenga hata kama ni mtoto wetu.

Ingawa Museven amelelewa na watanzania wakati akiendesha vita vya msituni vya kuiangusha serikali ya Unganda, lakini kwa vile ameota mapembe yanayomfanya aamue kuongoza nchi kwa mikono ya chuma, watanzania hatuna haja naye.

Nadhani pia ile ndoto ya kuwapo kwa shirikisho la nchi za Afrika Mashariki kwa maana ya kuungana kisiasa tuifute.

Hatuwezi kuungana kisiasa na kiuchumi na viongozi ambao wanaendesha nchi zao kihuni kihuni. Nadhani hatua tuliyoifikia ya kushirikiana katika ushuru wa forodha na mambo mengine yanatosha.

Watanzania kama tutajitia kimbele mbele cha kutaka kuungana na watu ambao hatuwajui vyema kama akina Museven ambao wanabadilika kama kinyonga, tutakuja kujuta.

Museven na uganda yake tuwaache waamue mambo yao na wakenya na Mwaki Kibaki wao tuwaache ugomvi wao wa ndizi na chungwa kuhusu katiba yao.

Tunajua wazi kuwa ingawa Tanzania tuna matatizo, lakini ya wenzetu Wanganda na Wakenya ni mazito zaidi.

Siamini kama rais wa Tanzania ajaye naye ataingia kucheza ngoma inayochezwa na Museven na Kibaki ya kutaka ushirikiano wa Afrika Mashariki bila kuelewa wenzake wanachezaje.

Kama ataingia kucheza ngoma asiyoijua ajue kuwa baada ya muda mfupi atapata matatizo makubwa ya ardhi, jeshi la watu wasiokuwa ajira na huenda watanzania wakakosa uvulimivu na kuingia mitaani kuandamana.

Alamsiki

0 Comments:

Post a Comment

<< Home