Mzee wa tafakari

Tuesday, February 06, 2007

Majeraha jumuia tuliyopaya 1977, bado hayajatupa somo?

WIKI hii Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala,aliwawaambia watanzania kwamba tume maalum ya iliyoundwa na serikali kukusanya maoni kuhusu Jumuia ya Afrika mashariki inatarajiwa kuanza kazi Oktoba 13 mwaka huu.

Kamala aliwataka waananchi kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu muundo wanaoutaka katika jumuia hiyo kabla ya kuanza rasimi kwa ushirikiano huo.

Aliwataka wadau wote wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini, mashirika yasiyo ya serikali, dola, wanasiasa na watu mbalimbali kushiriki katika kutoa maoni yao.

Dhima kuu ya kuundwa kwake ni kukusanya maoni ya wananchi wa Tanzania yatakayotumiwa kuboresha muundo na kazi za jumuiya hiyo kuelekea kwenye shirikisho.

Kamati hiyo itafanya shughuli zake kwa kipindi cha miezi sita, na itatembelea makao makuu ya mikoa na wilaya zote nchini.

Kwa hakika sasa nafasi ambayo watanzania walikuwa wakiitaka ya kushirikishwa katika ushiriki wa nchi yao katika jumuia ya Afrika Mashariki imewadia.

Ni wazi kwamba Watanzania watakaojitokeza mbele ya kamati hiyo watatoa maoni yao kwa kuzingaitia historia ya Tanzania na maslahi ya wananchi wenzao ambao hawatapata nafasi kama hiyo.

Sio jambo la siri kwamba watanzania wengi mpaka sasa hawaelewi sababu za Tanzania kuingia katika ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo mwaka 1977 ilivunjika na kuwapa hasara kubwa.

Pia mpaka sasa hawaelewi faida ambayo watapata iwapo Tanzania itagingia katika shirikisho kamili na kama makosa yaliyosababisha kuvunjika kwa jumuia iliyopita yamesahihishwa na nchi jirani za Kenya na Uganda.

Kwanza kabisa napenda kuwaeleza watanzania wenzagu kuwa waitumie fursa tuliyokuwa tunaisubiri ya kueleza msimamo wetu kuhusu shirikisho hili na kwamba tutoe maoni yetu kwa uwazi bila ya kumwogopa mtu.

Tanzania ni nchi yetu, haituwezi kuigawa kama pipi kwa mtu mwingine, ni vyema tukaridhia wenyewe uamuzi wowote tukaouchukua bila ya shikinizo kutoka kwa nchi yoyote au kwa taasisi fulani.

Kwa bahati mbaya, Watanzania wengi hupenda kutoa maoni baada ya uamuzi kuwa umeshapitishwa, ni vyema kwa sasa tujenge tabia ya kupenda kujua mambo na kutoa maoni yetu kwa wakati mwafaka.

Ajenda ya shirikisho inatakiwa kujadili katika maeneo yote kuanzia shuleni, misikitini, makanisani na hata kwenye baa. Na hata mijadala mikali ianzishwe na wasomi katika vyuo vya elimu ya juu kujadili suala hili nyeti.

Kwa ujumla ni kwamba watanzania tunapaswa kutafakari kwa makini zaidi kuhusu suala hili la kuingia katika jumuia ya Afrika Mashariki kutokana na historia ya jumuia hii. Jumuia hii haikuzaliwa leo ilikuwapo huko nyuma lakini watatu chache wakaiwekea mkono mchafu mpaka ikavunjika.

Tukirejea nyuma, tujiulize nani aliyevunja Afrika ya Mashiriki iliyopita? Ni dhahiri sio watanzania ni bali wenzetu Wakenya na Waganda kutokana na sababu zao za kisiasa.

Watanzania wakati huo chini ya utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere walionekana kama vile walikuwa wasindikizaji katika jumuia hiyo ndio maana hata walipotaka kuivunja walifanya hivyo kwa manufaa yao.

Kama ambavyo nimekuwa nikihoji siku zote je ni sababu zipi zimewafanya leo Wakenya na Waganda kuutaka ushirikano huu wa Afrika mashariki kwa nguvu zote tena? Nadhani watanzania tunapaswa kutafakari kwa makini vinginevyo hawa wenzetu watatugeuza kuwa mbuzi wa shughuli.

Hivi sasa wananchi wa nchi hizi tatu, ni sawa tumelala kitanda kimoja lakini kila mmoja anaota ndoto yake kuhusu jinsi atakavyofaidika na ushirikano huu.

Kwa vyovyote vile Wakenya wanawaza na kutamani shirikisho litakapoanza watamaliza matatizo yao ya ardhi, ukosefu wa ajira kupitia Tanzania na Uganda, Waganda hususan kiongozi wao Yoweri Museven wanapenda sana sifa, wao ndoto yao kubwa wanaota kuitawala Afrika Mashariki Mashariki.

Swali ambalo watanzania tunatakiwa kujiuliza ni kwamba wakati wenzetu wanawaza hayo, sisi Watanzania ajenda yetu inayotusukuma kuingia katika shirikisho hilo ni ipi? Ni kuwekeza katika nchi hizo? , sifa ya kuwa Afrika Mashariki tumeungana au ni ushabiki tu wa ngoma inayopita mtaani kwetu ambayo hatuijui madhumuni yake?

Kitu kingine ambacho watanzania tunapaswa kukijadili wanakati tunapotoa maoni yetu kuhusu shirikisho la Afrika Mashariki ni kuingia kwa nchi za Rwanda na Burundi katika Jumuia hiyo.

Wenzetu hawa wanajulikana bayana kutokana na nchi zao kukosa utulivu unaosabishwa na migogoro isiyoisha na ndani za nchi zao inayosababishwa na ukabila na uroho wa madaraka.

Baadhi ya watu wameaanza kuwa na wasiwasi kama ni vyema kuwa na watu kama hawa katika jumuia yetu. Ingawa wapo wanaosema kuwa huenda nchi hizo zikaiga ustarabu wa watanzania zikiwa ndani ya jumuia.

Kutokana na hali hiyo, tume maalum iliyoteuliwa kufanya kazi ya kukusanya maoni kuhusu Jumuia ya Afrika Mashariki nayo inapaswa kuwa makini ili isije ikatoa ripoti ambayo nyuma yake inashinikizo la mtu au nchi fulani.

Tunajua kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wa Kenya na Uganda wameanza kueleza kuwa Tanzania inasita kuingia katika jumuia kutokana na hofu ya ardhi kuchukuliwa na wageni. Kutokana na wenzetu hawa kujua hofu yetu wasije wakaitumia katika kushikiza ili mambo yao yaende wanavyotaka.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home